NGULI wa Masumbwi, Mike Tyson amezungumzia safari yake ya hivi karibuni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nchi ambayo ameitaja kama asili ya mababu zake alipowasili Nchini humo kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya pambano la kihistoria “Rumble in the Jungle”, lililowakutanisha mabondia maarufu Muhammad Ali na George Foreman mwaka 1974.
Katika chapisho lake rasmi la leo Oktoba 24, 2025 kwenye mitandao ya kijamii, Tyson ameweka picha kadhaa akiwa Jijini Kinshasa, ambako pia alialikwa kwa shughuli maalum za kitaifa na kitamaduni na kukutana na Rais wa DRC, President Félix Tshisekedi huku akielezea ziara hiyo kama uzoefu wa kubadilisha maisha akionyesha kupendezwa sana na nchi hiyo na watu wake na kuahidi kurejea tena Nchini humo.
Ujio wa bingwa huyo wa zamani wa uzito wa juu nchini DRC ulijumuisha ziara za kitamaduni na ushirikiano yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa michezo na burudani kati ya nchi hiyo na watu mashuhuri duniani. Mkutano wake na Rais Tshisekedi katika ikulu ya Kinshasa ulionekana kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukuza utalii na uwekezaji wa kimataifa nchini humo.
Mbali na ziara hiyo, Tyson aliwahi kusema anaamini asili yake ni kutoka Congo kwenye mahojiano ya kipindi cha Joe Rogan Podcast miaka michache iliyopita ambapo alisema “Ninaamini damu yangu inatoka Congo. Kuna kitu ndani yangu kinaniambia nipo nyumbani ninapokuwa Afrika”.