Na Prince Hoza Matua
WATU wanajiuliza nani mkubwa kicheo ndani ya klabu ya Simba SC kati ya Meneja mkuu na kocha mkuu, kwa maana ya Dimitar Pantev na Seleman Matola.
Hiyo yote inatokana na madaraka yao kikazi kugawanywa na Shirikisho la soka nchini, TFF, ambapo Shirikisho hilo halimtambui Pantev kama kocha mkuu na badala yake linamtambua Seleman Matola.
TFF kwa sheria zao linamtambua kocha mwenye leseni ya CAF A kusimama kwenye benchi la timu husika katika mashindano yake kwa maana Ligi Kuu bara, kombe la CRDB na Ngao ya Jamii.
Pantev hakidhi vigezo hivyo klabu ya Simba SC limemtambulisha kama meneja mkuu na badala yake Seleman Matola anahesabika kama kocha mkuu, mashabiki wa Simba SC wale wasioelewa wanachukulia Pantev kama mdogo wa Matola.
Na sasa Matola anaonekana kama kocha mkuu hivyo Simba SC haijafanya kitu chochote baada ya kuondoka Fadlu David's ambaye alikuwa kocha mkuu na Matola alikuwa kocha msaidizi namba tatu.
Fadlu wakati anajiunga na Simba, aliambatana na msaidizi wake, ingawa klabu ya Simba SC ilikuwa na kocha wake msaidizi ambaye ni Matola, Fadlu aliamua kuondoka Simba baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na viongozj wa klabu hiyo.
Fadlu aliondokea nchini Botswana wakati Simba ilipoenda kucheza na timu ya Gaborone United mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika raundi ya awali mchezo wa kwanza ambapo Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 goli ambalo lilisaidia kuwavusha raundi ya kwanza.
Simba iliingia raundi ya kwanza baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, timu ikinolewa na Hemed Morocco kwa muda.
Baada ya hapo uongozi wa Simba SC ulihaha kutafuta kocha mpya, ambapo Dimitar Pantev raia wa Burgalia alichukua mikoba ya Fadlu, Pantev alikuwa Meneja mkuu wa Gaborone United na alisifika kwa kuifundisha vizuri timu hiyo ingawa iliondoshwa na Simba katika raundi ya awali.
Aina ya uchezaji wake mzuri dhidi ya Simba, ilitosha kuwavutia wengi wakiwemo wachambuzi wa soka nchini na kuishauri Simba imchukue haraka baada ya kuondoka Fadlu, katika mchezo dhidi ya Simba na Gaborone, Pantev alifanya kazi kubwa Uwanjani na almanusura aitoe Simba.
Sare ya kufungana bao 1-1 kidogo iwaondoshe Simba katika mashindano, isipokuwa ushindi wa bao 1-0 ugenini iliwabeba Simba na kusonga mbele, kuanzia mechi ya kwanza jijini Gaborone na jijini Dar es Salaam, Pantev alitawala vipindi vyote.
Ilikuwa ngumu Simba kuleta kocha mwingine badala ya Pantev, kwa sababu Pantev alionekana ana uwezo mkubwa na Simba ilihitaji kocha mwenye uwezo mkubwa bila kujali wasifu wake.
Ingawa kwamba Simba ilikuwa na kocha Fadlu aliyeiwezesha timu hiyo kufika fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, kiwango cha Simba kilikuwa cha kawaida, lakini kwa ujio wa Pantev, ni dalili kwamba Simba imerejea kwenye kiwango chake.
Pantev ni kocha mzuri na ataweza kuifikisha katika mafanikio, kuhusu ukubwa kati yake na Matola ambaye atahesabika kama kocha mkuu na Pantev meneja mkuu, utofauti wao utabaki pale pale ila Pantev ambaye ni Meneja mkuu atakuwa mkubwa dhidi ya Matola ambaye ni kocha mkuu.
Pantev ana leseni A ya UEFA ambayo inamfanya asimame kama kocha mkuu kwenye michuano ya CAF, lakini kwenye mashindano ya ndani yanayotambuliwa na TFF atampisha Matola na Pantev atakuwa meneja mkuu.