TIMU ya Azam FC imetaka tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar katika mchezo wa marudiano wa Hatua ya 32 Bora leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Azam FC inakwenda Hatua ya makundi inayoshirikisha timu 16 kwa ushindi wa jumla wa 9-0 kufuatia ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Oktoba 18 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na winga Iddi Suleiman Ali ‘Nado’, mawili dakika ya 23 na 43, mshambuliaji Mkongo, Bola Jephte Kitambala mawili pia dakika ya 27 na 30, beki Paschal gaudence Msindo dakika ya 48 na Abdul Khamis Suleiman ‘Sopu’ mawili pia dakika ya 54 na 57.
Watoto wa Bilionea, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa – Abubakar Bakhresa na wadogo zake, Omar Bakhresa na Yussuf Bakhresa wamiliki wa Azam FC wote walikuwepo uwanjani kushuhudia mchezo timu ikiweka rekodi mpya katika historia yake.
Droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika itapangwa Jumatatu ya Novemba 3 katika studio za SuperSport Jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambao ni washirika wa Matangazo wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzia Saa 7:00 mchana.