WACHEZAJI wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wameingia kambini leo Jijini Dar es Salaam tayari kwa safari kwenda Jijini Brazaville, Kongo kesho kwa ajili ya mchezo wa Kundi E kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza na Kongo-Brazzaville Septemba 5 Uwanja wa Stade Alphonse Massemba-Débat Jijini Brazzaville kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Canada, Mexico na Marekani.
Baada ya hapo, Taifa Stars itarejea nyumbani kwa ajili ya mchezo mwingine wa kundi hilo kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger Septemba 9 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi E kwa pointi zake tisa, nyuma ya Morocco inayoongoza kwa pointi zake 15, wakati Kongo ambayo haina pointi inashika mkia baada ya timu zote kucheza mechi tano.
Kwa upande wao Niger wanashika nafasi ya nne kwa pointi zao sita za mechi nne nyuma ya Zambia yenye pointi sita pia za mechi tano.
Timu tisa zitakazoongoza makundi zitafuzu moja kwa moja kuiwakilisha kwenye Fainali za Kombe la Dunia, wakati washindi wa pili bora wanne wa makundi watamenyana katika Nusu Fainali na Fainali na mshindi atakwenda kushiriki mchujo wa Mabara kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia pia.
Mchujo wa Mabara, unaojulikana kama Inter-Confederation Play-Offs ni michuano mingine midogo inayoshirikisha timu sita za Mabara manne duniani, kasoro UEFA pamoja na nchi mwenyeji kutoka CONCACAF kutafuta timu mbili za mwisho za kushiriki michuano hiyo.