KLABU ya Simba imeachana na kipa wake, Ally Salim Juma Khatoro baada ya miaka nane tangu impandishe kutoka timu ya vijana.
Mlinda mlango huyo mzaliwa wa Pemba — alipandishwa kikosi cha kwanza Simba msimu wa 2017-2018 baada ya kufanya vizuri katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
Mara kadhaa alidaka mfululizo kama kipa namba moja baada ya makipa wa kwanza kuumia na msimu mzuri zaidi kwake ni wa 2022-2023 alipoiongoza Simba kufika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa kwa penalti 4-3 na Wydad Athletics ya Morocco kufuatia sare ya jumla ya 1-1 baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.
Aidha, Ally Salim ni mlinda mlango ambaye Simba haijawahi kupoteza mechi dhidi ya mtani, Yanga akiwa langoni na katika mechi mbili alizodaka zote Wekundu wa Msimbazi walishinda.
Mechi ya kwanza ilikuwa ni ya Ligi Kuu Aprili 16 mwaka 2023 Simba ikishinda 2-0, mabao ya beki Mkongo, Henock Inonga dakika ya pili na Kibu Denis dakika ya 32 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine ni Fainali ya Ngao ya Jamii Agosti 13 mwaka 2023 alipookoa penalti tatu Simba ikishinda kwa penalti 3-1 baada ya sare ya bila mabao Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Sifa nyingine ya Ally Salim ni kwamba pamoja na kuchukuliwa kama kipa wa akiba, lakini kila huduma yake ilipohitajika alifanya kazi yake vizuri.
Ni kwa sababu hiyo pia kuna wakati alikuwa anaaminiwa na kuwa kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars ambako pia alikuwa anafanya kazi yake vizuri.
Japokubwa taarifa haijathibitisha— lakini inaelezwa kipa huyo anajiunga na Namungo FC iliyoachana na Benni Kakolanya, kipa mwingine wa zamani wa Simba SC.