MWANDISHI wa Habari wa Ghana Soccernet, Nuhu Adam amesema Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024), iliyofanyika Tanzania, Kenya na Uganda ndiyo bora zaidi kwake tangu imeanza rasmi mwaka 2009.
"Hii ni hatua nzuri kwa nchi zote tatu ambazo zimeandaa michuano hii, nafikiri kwangu ndiyo mashindano bora zaidi kuwahi kutokea, CAF ilifanya kazi yake vizuri kwa kushirikiana na wenyeji, hivyo kiukweli ni jambo la kuvutia," amesema Nuhu.
Nuhu amesema sababu ya Shirikisho la Soka Africa (CAF), kuanzisha CHAN ni dalili nzuri ya kuandaa vizuri timu zote za ukanda wa Afrika kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya AFCON, ambayo ndio mikubwa zaidi kutokana na aina ya wachezaji.
"Siwezi kuzungumzia kasoro kwa sababu yapo mambo mengi yamefanyika kwa soka la Afrika Mashariki, timu kama Yanga, Simba kwa Tanzania, Gor Mahia ya Kenya zinafanya vizuri pia, hii ni dalili tosha ya jinsi nchi hizo tatu zilivyopiga hatua."
Aidha, Nuhu amesema licha ya maandalizi bora kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ila zinapaswa kuendelea kujiimarisha vizuri katika michuano ya Mataifa ya Afrika AFCON 2027, ambayo inahusisha nyota wengi wakubwa kutoka mataifa mbalimbali.
Nuhu amesema hayo leo Jumatatu ya Septemba 1, 2025, wakati akichangia mada katika Mwanaspoti X Space iliyoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), yenye mada isemayo, Tumekwama, tumepatia wapi CHAN 2024, nini kifanyike kwa ajili ya AFCON 2027.