TIMU ya kwanza ya Yanga leo imeshinda mabao 4-0 dhidi ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga A yote yamefungwa na wachezaji wapya, kiungo Lassine Kouma kutoka Stade Malien ya kwao, Mali, washambuliaji Muivory Coast, Ange Celestin Ecua kutoka Zoman FC ya kwao na Mkongo DR, Andy Bobwa Boyeli (24) kutoka Sekhukhune United FC ya Afrika Kusini na winga mzawa, Offen Francis Chikola kutoka Tabora United.
Yanga imekamilisha wiki moja tangu ianze mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya Jijini Dar es Salaam na wiki ijayo inatarajiwa kwenda Rwanda kwa maandalizi zaidi pamoja na mechi za kirafiki.