Timu ya Simba inatarajia kuhamisha kambi yake huko Misri kutoka mji wa Ismailia kwenda jijini Cairo kutokana na sababu mbalimbali zilizotajwa na benchi la ufundi la timu hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu kupitia tovuti ya Simba, Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema lengo la kuhamisha kambi kwenda Cairo ni kupata mechi nzuri za kirafiki zenye ushindani.
“Tarehe 15 tutahamisha kambi kutoka Ismailia hadi Cairo, ambako tutacheza mechi za kirafiki zenye ushindani ili kujiandaa ipasavyo. Kadri tunavyocheza mechi za kirafiki, wachezaji wapya na wa zamani wanazidi kuzoeana.
“Msimu uliopita tulikuwa vizuri kwenye Ligi Kuu, lakini kwenye Kombe la Shirikisho la CAF tulikosa ubora wa kutosha. Sasa tunapanda kiwango tunakwenda Ligi ya Mabingwa Afrika, tunahitaji kikosi chenye ushindani wa hali ya juu.
Hadi sasa Simba imeshafanya usajili wa wachezaji wapya saba, kati yao wanne ni wa kimataifa ambao ni Rushine De Reuck, Alassane Kante, Mohamed Bajaber na Jonathan Sowah wakati wengine watatu ni Watanzania ambao ni Morice Abraham, Hussein Semfuko na Anthony Mligo.