TIMU ya Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tabora United katika mchezo wa kirafiki leo Uwanja wa Gymkhana Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua na washambuliaji Mzimbabwe Prince Dube Mpumelelo na Ange Celestin Ecua aliyesajiliwa dirisha hili kutoka Zoman FC ya kwao, Ivory Coast.
Huo unakuwa mchezo wa nne wa kujipima nguvu kwa Yanga katika maandalizi ya msimu mpya na kuendeleza rekodi ya ushindi.
Mechi tatu za awali ilishinda 3-1 dhidi ya Rayon Sports Jijini Kigali nchini Rwanda, 2-1 dhidi ya Fountain Gate na 4-0 dhidi ya wadogo zao, U20 zote Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Msimu Yanga ipo chini ya Benchi jipya kabisa la Ufundi Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mfaransa Romain Folz na Msaidizi wake, Mspaniola Alejandro Manu Rodríguez Lázaro na Kocha wa Makipa, Majdi Mnasria.
Wengine ni Mtaalamu wa Viungo (Physiotherapist), Youssef Ammar wote kutoka Tunisia, Kocha wa Physic, Tshephang ‘Chyna’ Mokaila kutoka Botswana, Mchambuzi wa Video, Thula Bantu na Mkurugenzi wa Ufundi, Paul Matthews wote raia wa Afrika Kusini.
Yanga SC inatarajiwa kuuanza msimu kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba SC Septemba 16 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam – baada ya tamasha lake la kutambulisha kikosi cha msimu mpya, Kilele cha Wiki ya Mwananchi Septemba 12.