TANZANIA imeendeleza wimbi la ushindi katika Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania katika mchezo wa Kundi B usiku wa leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, beki wa kulia wa Simba SC, Shomari Salum Kapombe dakika ya 89 akimalizia krosi ya winga wa kushoto wa Azam FC, Iddi Suleiman Ali ‘Nado’.
Kwa ushindi huo Taifa Stars inafikisha pointi sita kufuatia ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Burkina Faso Jumamosi hapo hapo Uwanja wa Mkapa.
Mchezo mwingine wa Kundi B leo Burkina Faso imeshinda 4-2 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) hapo hapo Uwanja wa Mkapa.
Mabao ya Burkina Faso yamefungwa na Nasser Ouatarra dakika ya 11, Guiro dakika ya 61 kwa penalti, Malo dakika ya 78 kwa penalti pia na Baguian dakika ya 84, wakati ya CAR yamefungwa na Tchibinda dakika ya 15 na Zoumara dakika ya 90+5.
Burkina Faso inasogea nafasi ya pili nyuma ya Taifa Stars na mbele ya Madagascar na Mauritania zenye pointi moja kila moja na CAR inaendelea kushika mkia ikiwa haina pointi.