Na Prince Hoza Matua
SEPTEMBA 10 klabu ya Simba SC inaadhimisha tamasha lake ya Simba Day katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, katika siku hiyo Wekundu wa Msimbazi watacheza mechi ya kirafiki na timu ya Police FC ya Kenya.
Police FC ni mabingwa wa nchi hiyo na watawakilisha taifa hilo katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika kama ilivyo kwa Simba SC ambao wamemaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu bara msimu uliopita.
Katika tamasha hilo Simba SC watatumia nafasi hiyo ya kutambulisha jezi mpya, wachezaji wa kikosi chake cha msimu ujao na pia safi yake yote ikiwemo makocha.
Simba SC pia watatambulisha vikosi vyake vya timu za vijana kwa maana under-17 na under-20 pia timu ya wanawake, Simba Queens ambayo nayo imefanya usajili mkubwa kama ilivyo timu ya wanaume.
Kitu ambacho kinanifanya niandike makala hii ni kitendo cha klabu hiyo kuwaaga wachezaji wake wawili wa zamani wote wakiwa manahodha, John Raphael Bocco na Jonas Gelard Mkude.
Wachezaji hao waliichezea Simba kwa mafanikio makubwa lakini baadaye wakaachana na klabu hiyo na kutimkia vilabu vingine, Mkude yeye alidumu Simba misimu 13 na alijiunga Yanga SC ambao ni mahasimu wakuu wa Simba.
Na Bocco naye alidumu Simba misimu 8 na alitimkia JKT Tanzania, lakini uongozi wa Simba uliona umuhimu wa kuwapa heshima wachezaji hao na katika tamasha la Simba Day la mwaka huu wanawaaga rasmi.
Meneja wa Habari na mawasiliano Wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally amefunguka na kuthibitisha kuwa kwenye tamasha la Simba Day la mwaka huu itakuwa ni siku pia ya kuwaaga nyota wao wawili wa zamani wa kikosi hicho ambao ni Jonas Mkude na John Bocco.
Kwa ajili ya kutambua mchango wao ndani ya klabu hiyo ,huku pia akieleza kuwa mchezaji mwingine ambaye mashabiki wanamsubiri ataaagwa akimaliza pensheni yake japo hajataka kutaja jina lake.
"Tumeandaa utaratibu maalum wa kuwaaga wachezaji wetu vipenzi ambao waliitumikia Simba kwa muda mrefu lakini hatukupata bahati ya kuwaaga lakini niwaambie tumeshaongea nao na wamethibitisha watakuwepo Simba Day hii"
.
"Hapa namzungumzia John Bocco na Jonas Mkude ambao walikaa Simba kwa muda mrefu lakini wakaondoka bila Kuagwa, nitumie fursa hii kuwaambia kuwa Simba Day hii itakuwa ni siku maalum ya kuwaaga wachezaji hawa", alisema Ahmed Ally.
Bila shaka tamasha la Simba Day lakuvutia sana kutokana na utofauti wake lakini mimi binafsi nashindwa kuwaelewa Simba SC kama wameamua kufanya tamasha hili na kuwaaga wachezaji hao Bocco na Mkude kwa mapenzi mema kwa wachezaji hao au wanawadhihaki.
Mapenzi mema kwao ni kwa sababu wameona umuhimu wao na ndio maana wamewaita na kuwaaga mbele ya halaiki ya wapenzi na mashabiki wa Simba ulimwenguni kote, najua Mkude aliipigania Simba tangu akicheza Simba B na baadaye timu ya wakubwa.
Lakini Bocco naye alicheza kwa mafanikio na ndio maana wakampa kitambaa cha unahodha, dhihaka inakuja kwa uongozi wa Simba kuwaaga sasa na si huko nyuma, Mkude aliachana na Simba msimu juzi, na Simba wamefanya matamasha mawili mpaka sasa.
Na Bocco aliachana na Simba msimu jana, na Simba wamefanya tamasha moja bila Bocco, Simba walipaswa kuwaaga wachezaji hao kwa wakati wao na si sasa, kuwaaga wachezaji hao ni dhihaka za waziwazj na si kuonesha mapenzi kama wenyewe wanavyodhani.
ALAMSIKI