TIMU ya Senegal imefanikisha kumaliza nafasi ya tatu katika Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) kufuatia ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Sudan baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Taifa wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda leo.
Winga wa Al-Merrikh SC, Muhamed Tia Asad alianza kuifungia Sudan dakika ya sita, kabla ya beki wa Kati wa FC Gorée, Seyni Ndiaye kuisawazishia Senegal dakika ya 16.
Waliofunga penalti za Senegal ni Joseph Layousse, Issa Kane, Vieux Cissé na Libasse Guèye, wakati waliofunga za Sudan ni Mohamed Ahmed Saeed na Ahmed Tabanja pekee, huku Walieldin Khdir akipiga nje na ya Musab Makeen ikiokolewa na Marc Diouf.
Fainali ya CHAN 2024 itafuatia kesho kuanzia Saa 12:00 jioni baina ya Madagascar na Morocco Uwanja wa Moi International Sports Centre, Nairobi, Kenya.