MOROCCO itakutana na Tanzania katika Robo Fainali ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi A kufuatia ushindi wa 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jioni ya leo Uwanja wa Nyayo Jijini Nairobi nchini Kenya.
Mshambuliaji wa mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, RS Berkane, Oussama Lamlioui amefunga mabao mawili, dakika ya nane nafasi 80, wakati bao lingine amefunga Nahodha, Mohamed Rabie Hrimat kiungo wa AS FAR Rabat kwa penalti dakika ya 70.
Bao la kufuatia machozi la DRC limefungwa na mshambuliaji Jephté Kitambala Bola aliyesajiliwa Azam FC ya Tanzania akitokea AS Maniema ya kwao dakika ya 58.
Wenyeji, Kenya wameongoza Kundi A baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Zambia jioni ya leo bao la mshambuliaji wa Tusker FC, Ryan Wesley Ogam dakika ya 75 Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Jijini Nairobi.
Kwa matokeo hayo Harambee Stars wanamaliza na pointi 10 kileleni, hivyo watakutana na washindi wa pili wa Kundi B, Madagascar katika Robo Fainali Agosti 22 kuanzia Saa 11:00 jioni Uwanja wa Moi International Sports Centre, Nairobi.
Kwa upande wao Simba wa Atlasi waliomaliza na pointi tisa watakutana na vinara wa Kundi A, Tanzania katika Robo Fainali Ijumaa ya Agosti 22 pia Saa 2:00 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.