KLABU ya Yanga imemtambulisha beki wa kushoto Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anayejulikana pia kama
Zimbwe Junior kwa jina lingine la utani kama mchezaji wake mpya kuelekea msimu ujao.
Tshabalala anajiunga na Yanga kama
Mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Simba SC aliyoichezea kwa miaka 11 mfululizo.
Hussein alijifunga na Simba SC mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar ambako alicheza kwa msimu mmoja akitokea timu ya vijana ya Azam FC baada ya kuibukia klabu ya Friends Rangers ya Manzese.
Anakuwa mchezaji wa tisa baada ya viungo Lassine Kouma kutoka Stade Malien ya kwao, Mali, Mguinea, Balla Mousa Conte kutoka CS Sfaxien ya Tunisia, Mohamed Doumbia raia wa Ivory Coast aliyekuwa mchezaji huru na washambuliaji Mkongo DR, Andy Bobwa Boyeli (24) kutoka Sekhukhune United FC ya Afrika Kusini na Muivory Coast, Ange Celestin Ecua kutoka Zoman FC ya kwao.
Wengine ni wazawa, viungo wawili kutoka klabu za Ligi Kuu ya PBZ Zanzibar, Abdulnasir Mohamed Abdallah wa Mlandege na Nizar Abubakar Othman ‘Ninju’ wa JKU na winga Offen Francis Chikola kutoka Tabora United.