TIMU ya taifa Morocco imefanikitwa kutwaa Kombe la Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Madagascar usiku huu Uwanja wa Moi International Sports Centre, Kasarani, Nairobi nchini Kenya.
Ilikuwa mechi ya funga nikufunge, kabla ya mshambuliaji wa mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, RS Berkane – Oussama Lamlioui kufunga bao la ushindi dakika ya 82.
Hilo lilikuwa bao lake la pili kwa Lamlioui kwenye mchezo huo kufuatia kufunga lingine dakika ya 44 ambalo lilielekea kuwa la ushindi – kabla ya winga wa COSFAP Antananarivo, Toky Niaina Rakotondraibe kuisawazishia Madagascar dakika ya 68.
Madagascar ndio waliouanza vizuri mchezo huo na kupata bao la kuongoza kupita kwa mshambuliaji wa Fosa Juniors FC, Felicite Manohantsoa dakika ya tisa, kabla ya winga wa Renaissance de Berkane, Youssef Mehri kuisawazishia Morocco dakika ya 27.
Hilo linakuwa taji la tatu la CHAN kwa Morocco baada ya awali kulibeba katika mwaka 2018 na 2020, hivyo kuweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi Zaidi ubingwa wa michuano hiyo, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) waliobeba mara mbili, 2009 na 2016, wakati timu nyingine zilizowahi kutwaa taji la michuano hyo lililoanzishwa mwaka 2009 ni Tunisia mwaka 2011, Libya mwaka 2014 na Senegal mwaka 2022.
Aidha, Oussama Lamlioui ameibuka mfungaji wa michuano hiyo kwa mabao yake sita, huku nyota mwingine wa Morocco, kiungo wa ulinzi wa AS FAR Rabat, Mohamed Rabie Hrimat akibeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano na Kipa wa Teungueth FC, Marc Diouf akishinda Tuzo ya Kipa Bora na timu yake ya taifa, Senegal ikishinda Tuzo ya Mchezo wa Kiungwana.
Kwa ubingwa huo, Morocco wamezawadiwa fedha, Dola za Kimarekani Milioni 3.5 huku Madagascar wakiondoka na Dola Milioni 1.2 kwa kumaliza nafasi ya Pili.