KLABU ya Simba SC imemtambulisha beki wa kushoto, Anthony Richard Mligo ambaye Agosti 6 atatimiza miaka 18 kutoka Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi kuwa mchezaji wake mpya kuelekea msimu ujao.
Baada ya kukamilisha usajili wake, Mligo anapanda ndege leo kwenda mjini Ismailia nchini Misri kuungana na wezake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Mligo ni mchezaji aliyeibukia klabu ya Geita Gold msimu wa 2023/2024, kabla ya kuhamia Namungo FC msimu uliopita ambako aliendelea kufanya vizuri na kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’.
Chipukizi huyo alikuwemo kwenye kikosi cha Tanzania kilichotwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya umri wa miaka 20, CECAFA U20 Oktoba mwaka jana nchini akiibukia mfungaji wa michuno hiyo.
Chipukizi huyo alikuwepo pia kwenye kikosi hicho cha Ngorongoro Heroes kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) U20 nchini Misri.
Anakuwa mchezaji mpya wa saba kutambulishwa rasmi Simba SC hadi sasa baada ya beki wa kati, Rushine De Reuck (29) kutoka Mamelodi Sundowns ya kwao, Afrika Kusini, kiungo Msenegal, Alassane Maodo Kanté (24) kutoka CA Bizertin ya Tunisia, winga Mohammed Omar Ali Bajaber kutoka Polisi ya kwao, Kenya na mshambuliaji Mghana, Jonathan Sowah kutoka Singida Black Stars ya nchini.
Wengine ni wazawa, kiungo Hussein Daudi Semfuko (21) kutoka Coastal Union ya Tanga na mshambuliaji Morice Michael Abraham (21) Spartak Subotica ya Serbia.
Simba inatarajiwa kuuanza msimu kwa michuano midogo ya Ngao ya Jamii maalum kuashiria upenuzi wa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, 2025/2026 inayotarajiwa kufanyika kati ya Septemba 11 hadi 14.
Simba SC itacheza na Singida Black Stars. Septemba 11 na ikishinda itakutana na mshindi kati ya Yanga na Azam FC katika Fainali.
Baada ya hapo Simba itaingia kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambayo itaanza Septemba 16 – wastani wa wiki mbili tu baada ya kumalizika kwa na Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).