WENYEJI, Kenya ‘Harambee Stars’ wameweka hai matumaini ya kwenda Robo Fainali ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco ‘Simba wa Atlasi’ katika mchezo wa Kundi A leo Uwanja wa Moi International Sports Centre, Nairobi.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji wa Tusker FC, Ryan Wesley Ogam dakika ya 42 akimtungua kipa wa Raja Athletic, maarufu kama Raja Casablanca.
Lakini haukuwa ushindi mwepesi kwa wenyeji, kwani walilazimika kucheza pungufu kipindi chote cha pili baada ya kiungo wake wa ulinzi, Chrispine Erambo wa Tusker pia kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 45’+4.
Mchezo mwingine wa Kundi A leo Angola imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zambia Uwanja wa Taifa wa Nyayo hapo hapo Nairobi.
Mabao yote ya Palancas Negras yamefungwa na mshambuliaji wa Interclube, João Chingando Manha ‘Caporal’ dakika ya 79 na 86, wakati bao pekee la Chipolopolo limefungwa na beki wa Kabwe Warriors, Dominic Chanda dakika ya 73.
Baada ya mechi za leo, Kenya inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Angola pointi nne kufuatia timu zote kucheza mechi tatu, wakati Morocco na pointi tatu sawa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya wote kucheza mechi mbili sawa na Zambia inayoshika kufuatia kufungwa mechi zote mbili za awali.