Mkongwe wa Mziki nchini Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone amevunja ukimya kuhusu mwenendo wa talaka yake na Mke wake Daniella Atim waliofunga ndoa miaka 17 iliyopita na kusisitiza kuwa ingawa amekubali mali zake kugawanywa lakini hakubaliani na kitendo cha kulazimishwa kusaini wosia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Vyombo vya Habari Nchini Uganda vya BigEye na Pulse Uganda, Chameleone amesema hayo wakati akiwa LIVE kupitia kurasa zake Mtandaoni na kuweka wazi kuwa mali wanazogombea na Mkewe ni mali za Watoto na sio zao binafsi.
“Mambo tunayopigania ni ya Watoto sio yetu na hata Watoto watawaachia Watoto wao, acha kutengeneza hali ambayo hakuna" amesema Chameleone.
Mchakato wa kugawanywa kwa mali zake umeanza kuonekana mapema baada ya Mke wake kufungua mashtaka Mahakamani kudai talaka mnamo mwezi Machi mwaka huu ambapo August 21 alikubali kutoa talaka kwa kile Mkewe alichokiita kutelekezwa.
Chameleone mwenyewe amesema kuwa hana pingamizi la kusaini hati za kisheria ikiwa sheria itamtaka na amesisitiza kuwa utajiri wake wote ni kwa manufaa ya Watoto wake watano na sio yeye wala Mkewe na ameongeza kwamba hajalemewa na mchakato wa talaka amewahakikishia Mashabiki zake kuwa bado yuko katika amani wakati vita ya kisheria ikiendelea.