Na Prince Hoza
ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Job Yustino Ndugai amefariki Dunia August 06,2025 akiwa anaendelea kupatiwa matibabu Hospitalini baada ya kuugua ghafla.
Ndugai amekuwa Spika wa Bunge tangu November 17, 2015 hadi Januari 06, 2022 alipojiuzulu na kuendelea kuwa Mbunge wa Kongwa nafasi ambayo ameendelea kuitetea kwa kuchukua fomu tena mwaka huu ambapo ameshinda kwenye kura za maoni.
Ndugai ambaye amezaliwa January 22,1960 alishinda kura za maoni za Ubunge wa Jimbo la Kongwa kwa kupata kura 5690.
ALIHAKIKISHA TAIFA STARS INAFUZU FAINALI ZA AFCON MWAKA 2019
Ndugai tutamkumbuka kwenye tasnia ya michezo hasa alipokuwa Spika wa Jamhuri ya Muungano ambapo alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha soka la Tanzania linapiga hatua.
Ikumbukwe marehemu Ndugai alikuwa sambamba na wabunge wenzake kuunda Kamati ya hamasa ambayo iliisaidia timu ya taifa kufuzu fainali za Afrika, mwaka 2019 Taifa Stars ilifuzu fainali za mataifa Afrika, AFCON zilizofanyika nchini Misri.
Nakumbuka mheshimiwa Ndugai alipambana vilivyo kuona wachezaji wa Taifa Stars wanapata stahiki zao ambazo zikasaidia kufuzu fainali, wakati hup Rais wa Jamhuri ya Muungano alikuwa Dkt John Pombe Magufuli ambaye naye ni marehemu.
ALIKUWA SHABIKI KINDAKINDAKI WA SIMBA SC
Kwa ushirikiano wao viongozi wa Tanzania, kwa maana Rais wa nchi na Spika wa nchi walihalikisha Tanzania inafuzu fainali za mwaka huo (2019) baada ya miaka 38 ilipofanya hivyo mwaka 1981 wakati fainali zake zilipofanyika nchini Nigeria.
Marehemu Ndugai atakumbukwa kwa juhudi zake kwenye michezo kwani mbali ya kulisaidia taifa katika michezo, pia alikuwa shabiki kindakindaki wa klabu ya Simba SC.
Ndugai alishiriki kuanzisha tawi la Simba SC jijiji Dodoma ambalo liliwahusu waheshimiwa wabunge, tawi hilo lilizinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye kwasasa ni Rais.
YEYE NA RAIS MAGUFULI WALIWAPA VIWANJA WACHEZAJI WA STARS KWA KUFUZU
Kwa kifupi marehemu Ndugai alikuwa na mchango mkubwa kwenye soka na kifo chake ni pigo, Watanzania tumempoteza mtu muhimu na MIKASI imeona umuhimu wake na kuandika kumbukizi kwa ufupi.
Baada ya Stars kufuzu fainali za mwaka 2019, Rais Magufuli aliamua kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo ya taifa viwanja mjini Dodoma, Ndugai ambaye ni Spika, alishiriki kikamilifu kuhakikisha wachezaji wa timu hiyo wanapewa viwanja vyao.
Tanzania imepata bahati kubwa ya kuwa na viongozi wa kisiasa ambao ni wapenda michezo, kwani Ndugai alikuwa mwanamichezo kindakindaki, kifo chake kimetushitua sana sisi wadau na mwisho tunamshukuru mwenyezi Mungu.
ACKSON TULIA AMLILIA
Taarifa ya kifo hicho zilitolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson.
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma,” amesema Tulia katika taarifa hiyo na kuongeza
“Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Spika.
Aidha amesema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya Marehemu inaratibu mipango ya mazishina taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.