Baada ya Simba Queens kutangaza kuachana na mshambuliaji raia wa Kenya, Jentrix Shikangwa inadaiwa yupo njiani kurejeshwa kikosini kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na michuano mingine ya ndani ya soka la wanawake.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Simba Queens, amesema wameamua kumrejesha kikosini kutokana na uhitaji wake na kile alichokifanya ndani ya misimu mitatu.
“Kulikuwa na changamoto kidogo ya uamuzi na ni kama tulikurupuka, lakini maoni ya mashabiki mitandaoni yametuamsha kwa sababu wao pia wanahusika na hii timu,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Viongozi wakubwa waliuliza shida nini, tukasema mchezaji alitaka kiasi kikubwa cha pesa, wakasema mpatieni hiyo fedha kwa sababu ni mchezaji muhimu kwetu na amefanya makubwa.” Amesema Kiongozi huyo
Julai 15 mwaka huu, Simba ilitangaza kuachana na mshambuliaji huyo wa zamani wa Vihiga Queens na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Starlets, akiwa miongoni na nyota 13 walioitumikia msimu uliopita.
Shikangwa ndani ya misimu mitatu aliyocheza Simba, msimu wa kwanza tu aliipa timu hiyo ubingwa na akaibuka mfungaji bora akifunga mabao 17, uliofuata akamaliza na mabao manane akicheza mechi nane na msimu huu akamaliza na mabao 24.