Mkurugenzi Mtendaji wa Manara TV Haji Manara amekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa mitandaoni kwamba anatarajia kurejea kufanya kazi katika klabu ya Simba SC.
Akizungumza na Manara Tv, Manara amesema, "Nimeona na mimi nimetumiwa mitandaoni kwamba naenda tena kufanya kazi Simba, na watu wengi mmeniuliza. Jawabu langu ni Uongo, sina mpango huo kwa sasa mimi naendelea kuwa mshabiki na mwanachama wa Yanga ingawa niko mbali na mambo haya kwa sasa lakini bado nafuatilia kwa karibu kila kinachoendelea ndani ya klabu yangu, nalipa ada za uanachama," alisema Manara na kuongeza kuwa;
"Ni kweli nliwahi kufanya kazi Simba lakini siwezi kurudi na moyo wangu uko Yanga, hata kama kwa sasa sifanyi kazi Yanga lakini moyo wangu uko Yanga na niwaombe wanachama na washabiki wa Yanga wapuuze hadithi za mitandaoni ambazo wakati mwingine zina lengo ovu, zina lengo baya dhidi yangu na hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi mkuu wa Oktoba ambao mimi nagombea nafasi ya Udiwani Kariakoo," alisema Manara.
Aidha, Manara amewasihi wanachama na mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika kilele cha Wiki ya Yanga na kununua jezi za klabu hiyo akibainisha kuwa zina ubora wa hali ya juu.