KAMPUNI ya michezo ya Kubahatisha, Betika imedhamini michuano ya Klabu za Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame Cup 2025 inayotarajiwa kuanza Septemba 2 hadi 15 Jijini Dar es Salaam kwa dau la Shilingi Milioni 42 za Kenya, Zaidi ya Shilingi Milioni 813.9 za Tanzania.
Mkataba baina ya Betika na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) umesainiwa leo Jijini Nairobi nchini Kenya ukishuhudiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Wallace John Karia ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CECAFA, Mama Doris Petra.
Mtendaji Mkuu wa Betika, Mutua Mutava amesema katika hafla hiyo kwamba wamedhamini michuano hiyo kutokana na Imani yao katika maendeleo ya soka ya ukanda wa CECAFA.
Katika droo iliyopangwa leo hoteli ya Pan Pacific Suites Jijini Nairobi, wenyeji Singida Black Stars FC wamepangwa Kundi A pamoja na Garde Cotes FC ya Djibouti, Coffee SC ya Ethiopia na Polisi FC ya Kenya.