KLABU ya Azam imeendelea kuboresha benchi lake la Ufundi kwa kuajiri kocha mwingine Msaidizi, Anicet Kiazayidi Makiadi (33) ambaye anaungana na Mkongo mwenzake, Kocha Mkuu, Jean-Flotent Ibenge.
Anicet Kiazayidi Makiadi anajiunga na Azam FC baada ya kuiwezesha Aigles du Congo kutwaa ubingwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama Kocha Mkuu.
Kabla ya kujiunga na Aigles du Congo, Kiazayidi aliifundisha kwa miezi mitatu Tabora United akichukua nafasi ya Mkenya, Francis Kimanzi aliyeondolewa kwa matokeo mabaya.
Ni wakati huo alijitengenezea umaarufu Tanzania baada ya kuiwezesha Tabora United kufanya vizuri ikiwemo kuwafunga mabingwa wa nchi, Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Awali, Kiazayidi alikuwa Kocha Msaidizi wa timu za AS Vita Club chini ya Ibenge kati ya 2017 na 2019, Maniema Union chini ya Guy Lusadisu Basisila kati ya 2019 na 2021 na AS Simba kati ya 2022 na 2023 chini ya Mspaniola, Julio César Gómez.