MSHAMBULIAJI Mghana, Jonathan Sowah (26) amejiunga na Simba SC akitokea Singida Black Stars alikodumu kwa nusu msimu tangu awasili.
Taarifa ya Singida Black Stars leo imesema kwamba wameridhia kumruhusu Sowah kujiunga na Simba SC baada ya mazungumzo baina ya watu wenye mamlaka ya juu kwenye timu zote.
Hao ni Mlezi wa Singida Black Stars, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohamed Gulam ‘Mo’ Dewji ambaye pia ni Rais wa heshima wa klabu hiyo.
Sowah alijiunga na Singida Black Stars Januari 17, mwaka huu 2025 akitokea Al-Nasr ya Libya ambako alidumu kwa msimu mmoja baada ya kuwasili akitokea Medeama ya kwao, Ghana Januari 27, mwaka jana 2024.
Kisoka, haswa Sowah aliibukia Danbort FC ya kwao pia, Ghana kabla ya kuhamia Medeama SC Novemba 11, mwaka juzi, 2023.
Akiwa Medeama ndipo Watanzania walianza kumuona mchezaji huyo kufuatia klabu yake hiyo kukutana na Yanga ambao ni wapinzani wakubwa wa Simba nchini katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga ilikuwa timu ya kwanza kuonyesha nia ya kumsajili Sowah kabla hajaenda Al-Nasr, lakini mapema mwaka huu akajiunga na Singida Black Stars huku kukiwa na taarifa kwamba atacheza kwa muda kabla ya kujiunga na Wananchi.
Inaaminika rekodi yake ya utovu wa nidhamu ilichangia Yanga kuachana na mpango wa kumsajili baada ya kugombana na mashabiki wa Simba mara mbili mfululizo katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam na Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Aidha, kitendo cha kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi muhimu ya Fainali ya Kombe la TFF, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB kilionekana kabisa kuwafanya Yanga wajifikirie mara mbili kumsajili mchezaji huyo licha ya rekodi yake nzuri ya kufunga mabao.