MSHAMBULIAJI wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva (31) amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu ya Al-Talaba SC ya Iraq.
Taarifa ya Al-Talaba, klabu yenye maskani yake mjini Al-Rusafa Jijini Baghdad imesema kwa kifupi mno; “Mtanzania Simon Masova amesaini mkataba mpya,”.
Msuva alijiunga na washindi hao wa mataji matano ya Ligi Kuu ya Iraq ‘Iraq Stars League’ Mei 8 mwaka 2024 akitokea Al-Najma ya Saudi Arabia ambako alicheza kwa nusu msimu akitokea JS Kabylie ya Algeria iliyomsajili Desemba 19 mwaka 2023.
Msuva aliwasili JS Kabylie akitokea Al-Qadsiah ya Saudi Arabia aliyojiunga nayo Agosti 28 mwaka 2023 baada ya kuondoka Wydad Athletic ya Morocco aliyojiunga nayo Julai 24 mwaka 2022.
Difaa El Jadida ndio klabu iliyomtambulisha Msuva katika soka ya Morocco baada ya kumsajili OKtoba 11, mwaka 2020 kutoka Yanga ya nyumbani, Dar es Salaam.