KLABU ya Simba imemtambulisha kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Morice Michael Abraham (21) kuwa mchezaji wake mpya baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Spartak Subotica ya Serbia.
Abraham ni mchezaji aliyeibukia katika akademi ya Alliance ya Mwanza, kabla ya kwenda Spartak Subotica mwaka 2021 alikoanzia kucheza timu ya vijana, kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa – na mwaka jana akapelekwa kwa mkopo RFK Novi Sad ya Serbia pia.
Ikumbukwe jana Simba ilimtambulisha kiungo Msenegal, Alassane Maodo Kanté (24) kuwa mchezaji wake mpya kuelekea msimu ujao akitokea CA Bizertin ya Tunisia.
Kante ni mchezaji aliyeibukia katika klabu ya US Gorée ya kwao, Senegal mwaka 2019 kabla ya kwenda CA Bizertin mwaka 2022.
Wanafanya idadi ya wachezaji wapya watatu waliotambulishwa rasmi Simba SC hadi sasa – baada ya beki wa kati wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck (29) anayeweza pia kucheza kama kiungo wa ulinzi pia kutoka Mamelodi Sundowns ya kwao.
Lakini tayari imethibitika pia Simba SC imekamilisha usajili wa mshambuliaji Mghana, Jonathan Sowah (26) kutoka Singida Black Stars.