REFA Ahmed Arajiga wa Manyara ndiye atakayechezesha Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB kesho baina ya Yanga SC ya Dar es Salaam na Singida Black Stars ya Singida kuanzia Saa 2:00 usiku Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Arajiga atasaidiwa na Frank Komba wa Dar es Salaam na Hamdani Said wa Mtwara watakaokuwa wakikimbia na vibendera pembezoni mwa Uwanja, wakati refa wa nne mezani atakuwa ni Tatu Malogo wa Tanga, Kamishna Zakayo Mjema wa Arusha na Mtathmini wa Marefa, Victor Mwandike wa Mtwara.
Yanga SC kesho wanataka kumalizia msimu mzuri katika mashindano kwa kutwaa taji la nne baada ya Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano na Ligi Kuu na la tano kwa ujumla pamoja na Kombe la Toyota nchini Afrika Kusini, michuano ambayo ilishirikisha timu za Augsburg ya Ujerumani na wenyeji, TS Galaxy na Kaizer Chiefs.
Kwa Singida Black Stars watakuwa wanataka kushinda taji la kwanza kabisa katika historia yao, wakiwa na kumbukumbu ya kulikosa taji hilo mwaka 2018 wakati huo timu ikijulikana kama Singida United baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakati huo michuano ikijulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).