Klabu ya Yanga SC imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Kombe la Muungano 2025 baada ya kuifunga JKU ya Zanzibar bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Mei 1, 2025, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli, katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza.
Kwa ushindi huo, Yanga walijinyakulia Kombe pamoja na zawadi ya shilingi milioni 50, huku JKU wakipata milioni 30 kama washindi wa pili. Zawadi hizo zilikuwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha na kuendeleza michezo nchini, na zilikabidhiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid.
Mashindano ya Kombe la Muungano yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kupitia michezo. Ushiriki wa timu kutoka pande zote mbili za Muungano umeonyesha dhamira ya pamoja ya kukuza vipaji na kuendeleza michezo kama chombo cha kuleta umoja na maendeleo ya kijamii.
Yanga SC imewahi kutwaa Kombe la Muungano mara 7 katika historia ya michuano hiyo. Mataji hayo yalipatikana katika miaka ya 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000 na leo 2025
Simba SC nayo inashika nafasi ya pili kwa kutwaa mara nyingi Kombe hilo mara 6 ambapo mara ya mwisho ilishinda mwaka jana 2024 mbele ya Azam FC.
