NDOTO za Simba SC kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika hazikutimia leo baada ya kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco katika mchezo wa marudiano wa Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Matokeo hayo yanamaanisha RSB Berkane wanatwaa taji la CAF Confederation Cup kwa ushindi wa jumla wa 3-1 kufuatia kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa Manispaa ya Berkane mjini Berkane.
Katika mchezo wa leo Simba SC walitangulia kwa bao la Mzambia, Joshua Mutale Budo dakika ya 17 akimalizia pasi ya winga mwenzake, Mkongo Elie Mpanzu Kibisawala – kabla ya kiungo wa Kimataifa wa Mali, Soumaila Sidibe kuisawazishia RSB Berkane dakika ya 90’+3.