Na Prince Hoza
WAKATI Yanga SC ikilazimishwa sare tasa 0-0 na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu bara uwanja wa Meja Isamuyo uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam niliandika makala kwenye safu hii nikimponda vibaya kocha mkuu wa Yanga Miloud Hamdi.
Nakumbuka hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza baada ya kupewa mikoba kutoka kwa mtangulizi wake Sead Ramovic, Hamdi alitambulishwa siku moja baada ya Ramovic kuacha kazi na kila mmoja alilalamika sana mabadiliko ya Yanga.
Ramovic raia wa Ujerumani, aliacha kazi Yanga aliyeifundisha muda mfupi akichukua nafasi ya Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina aliyetimuliwa.
Mjerumani huyo aliyekuwa anaifundisha timu ya TS Galaxy ya Afrika Kusini, aliamua kuacha kazi Yanga baada ya kupata ajira kubwa kwenye klabu ya CS Belouizdad ya Algeria.
Ramovic alipochukua mikoba ya Gamondi ambaye msimu uliopita alifanya mambo makubwa ikiwemo kutetea ubingwa wa bara, kombe la CRDB Cup na kuiwezesha Yanga kwa mara ya kwanza kutinga robo fainali ya Ligi ya mabingwa barani Afrika.
Yanga ya msimu uliopita ilikuwa hakamatiki kwani kama si mwamuzi kukataa bao la Stephanie Aziz Ki alilolifunga dhidi ya Mamelodi Sundown's ya Afrika Kusini kwa vyovyote Yanga ingetinga nusu fainali.
Gamondi pia alisifika kwa mchezo mzuri huku Yanga ikitumia nguvu na akili kwani wachezaji wake walikuwa na kasi sana, ushindi mkubwa wa mabao matano yalikuwa ya kawaida, hata mtani wake Simba SC alikoga 5-1.
Lakini msimu huu haukuwa mzuri kwake, licha kwamba alianxs vema msimu kwa kushinda Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba bao 1-0, na pia akianza ligi vema kwa ushindi wa mechi nane mfululizo.
Timu ya Gamondi iliweka rekodi ya kucheza mechi 8 bila kuruhusu bao, wachambuzi walianza kumshambulia Gamondi wakidai timu yake haichezi kandanda la kuvutia kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Na Yanga ya Gamondi ya msimu huu ilionekana wazi wazi kwamba haichezi vizuri, vipigo viwili mfululizo dhidi ya Azam FC 1-0 na baadaye 3-1 dhidi ya Tabora United.
Uongozi wa Yanga chini ya Rais wake Injinia Hersi Said uliamua kumfuta kazi Muargentina huyo aliyopata pia kuzinoa timu mbalimbali barani Afrika ikiwemo Mamelodi Sundown's na CS Belouizdad.
Alipoondoka Gamondi, akaja Ramovic ambaye hakuwa na umaarufu wowote nchini Tanzania, Ramovic alikutana na vipigo viwili mfululizo dhidi ya Al Hilal 2-0 na MC Alger 2-0 kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika.
Sio siri kushindwa kwa Yanga kimataifa msimu huu kumetokana na mabadiliko hayo ya ghafla, lakini kwenye Ligi Kuu bara, Ramovic alisifika na kikosi chake kikawa kinatoa dozi, Yanga ikabadilishwa jina na sasa ikawa onaitwa "Gusa achia twende kwao".
Chakushangaza Ramovic akatimka na akatangazwa kocha mpya raia wa Algeria, Miloud Hamdi, kabla ya kutua Yanga, Hamdi alikuwa anainoa Singida Black Stars.
Ikiwa chini ya Hamdi, Yanga ikaanza na sare dhidi ya JKT Tanzania, nikiwa kwenye meza nikachukua kalamu na karatasi na kuandika makala ambayo haikuwa nzuri, kwani nilimponda waziwazi Hamdi nikidai si kocha wa mafanikio kwa Yanga.
Leo nadiriki kumwamkia "Shikamoo Miloud Hamdi", najua anastahili Shikamoo yangu kwakuwa amenizidi umri, kwani yeye ana umri wa miaka 53, akizaliwa Juni, 1971, Hamdi ni bonge la kocha aisee, sijaziona sifa zake kwa Wanahabari, lakini ni bonge la kocha.
Yanga imerudi zama za Gamondi wa msimu uliopita, ingawa timu hajaanza nayo, lakini anakwenda kutetea mataji, Ligi Kuu bara na kombe la CRDB, endapo Yanga watampa nafasi tena aiongoze timu hiyo ninaamini michuano ya kimataifa itafika mbali sana.
ALAMSIKI
