Kwenye kipindi cha Crown FM - Air 20, Alikiba amefunguka kuhusu sababu ya kutowahi kufanya tena kolabo na Lady Jay Dee.
Ingawa haijawahi kufahamika wazi chanzo, Alikiba anasema tayari walishakutana hata baada ya Lady Jay Dee kusema hafikirii kolabo kati yao tena, lakini hajui ni nini hasa kilichompelekea dada huyo kutoa kauli ya kutoshirikiana naye tena.
Akizungumzia moja ya nyimbo zake kubwa zaidi, Seduce Me, Alikiba alisema wazo la wimbo huo lilitokana na mahusiano yake ya zamani na mpenzi wake ambaye kwa sasa ni mheshimiwa. Alikiba alisema mpenzi huyo alipenda sana kutumia Kiingereza na wakati fulani wakiwa pamoja kwa producer Man Water, alianza kuzungumza kwa lafudhi ya Kiingereza na kutamka maneno kama "Seduce Me"—ambapo Alikiba alianza kuimba hapo hapo. "Kila kitu huwa nachukulia kama fursa kwenye muziki wangu," alisema.
Alikiba alisimulia kuhusu mpenzi wake mwingine aliyemfundisha kifaransa. “Alinipigia nikiwa studio, nikamwambia anicheki baadaye maana nina rekodi. Nikamwomba maneno ya Kifaransa, akanitumia maandishi na voice note. Hivyo ndivyo wimbo wa Aje ilivyozaliwa.” Wimbo huo ulimpa tuzo ya MTVEMA na video yake ndio ilikuwa ya gharama zaidi kuwahi kufanya, ikigharimu dola 36,000.
Kuhusu biashara, Alikiba alieleza changamoto alizokutana nazo kwenye bidhaa za Mofaya. Alisema mkataba haukuwa sawa hasa upande wa kuingiza bidhaa kutoka Afrika Kusini na pia kutopatiwa kanuni ya bidhaa. “Nilizuia kwa sababu mkataba haukuwa unaenda sawa. Mungu akijalia mzigo utakuja.”
Kuhusu maisha binafsi, Alikiba alikanusha kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Queen Darlin. Alisema walikuwa tu marafiki wa karibu, na dada huyo alikuwa sehemu ya watu waliomuunga mkono sana mwanzo. “Tulipendana kama dada na kaka. Sasa hivi hatuna ukaribu kama zamani.”
Kuhusu Killy na Cheed, Alikiba alifananisha Kings Music na chuo. Alisema msanii anapoondoka ni kama amehitimu, hivyo si sahihi kurudi tena. “Wameshajitambulisha kama wasanii wanaojitegemea. Wasivunjike moyo.”
Alikiba alifafanua tukio la Abdu Kiba kukutana na Diamond Platnumz. Alisisitiza hakuwa na kinyongo, 'halikuwa kosa'.
(SNS)
