Taifa Stars ilijiandaa kufungwa...

Na Prince Hoza

MABAO ya Simba wa Atlasi yaliyoizamisha Taifa Stars yamefumgwa na nyota wa La Liga, beki wa Real Sociedad, Nayef Aguerd dakika ya 51' na kiungo wa Real Madrid, Brahim Díaz kwa Penalti dakika ya 58 Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Oujda. 

Hicho ni kipigo ilichokipata Taifa Stars dhidi ya Morocco, kipigo ambacho kimewasononesha Watanzania wengi, matumaini ya Tanzania kutinga fainali za kombe la dunia yanawekwa shakani na kipigo hicho.

Morocco si daraja letu kiasi kwamba kufungwa ni kama dhambi, hapana Morocco ni timu ya kiwango cha juu sana ambapo ni mapema sana kuifikia na kuiweka chini.

Malalamiko kufungwa na Morocco yanakuja kwamba hakukuwa na maandalizi hata kidogo kuelekea mchezo nao, Iko tofauti na mechi nyingine Taifa Stars inajiandaa vya kutosha, lakini mechi dhidi ya Morocco hakuna maandalizi kabisa.

Nashangaa kuona mchezo mkubwa wa kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Morocco, Taifa Stars inasafiri pasipo hamasa yoyote, nilichokiona kwa Taifa Stars ni sifa nyingi zikielekezwa kwa mtawala Wallace Karia


Shirikisho la soka nchini TFF kila kukicha lilikuwa lilipeleka sifa Kwa Karia kutokana na mafanikio aliyopata, hakukuwa na hamasa ya kuelekea kwenye mchezo huo, kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Morocco nimeona kama tulistahili.

Maendeleo ya timu yetu ya taifa, Taifa Stars ni duni sana ingawa hilo alionekana kutokana na mazuri yanaonekana kwenye vilabu vyetu, Simba na Yanga zimekuwa bora na kufanya kwake vizuri Tanzania inazidi kumwagiwa sifa kemkem.

Inasikitisha sana timu yetu ya taifa ikishindwa kufuzu fainali za kombe la dunia ingawa malengo yetu ni kufuzu, mbali na kufuzu fainali za kombe la dunia, timu ya taifa, Taifa Stars haifiki mbali kwenye fainali za kombe la mataifa Afrika, AFCON.

Timu hiyo imefuzu mara tatu lakini zote ikiishia hatua ya mtoano, kwa ukubwa tulinao kama nchi, tulistahili kufika robo fainali au nusu fainali, lakini tunaweza kufika fainali ama kuchukua ubingwa kabisa.

Kitendo cha Stars kuishia hatua ya makundi haifurahishi hata kidogo, vile vile Shirikisho letu kwa maana TFF alisikii uchungu na timu yake, kitendo cha kukataa kunolewa na makocha wa kigeni ni dhahiri kwamba hawataki mafanikio.

Bado Watanzania kunolewa na makocha wazawa kwa maana kwamba nchi yetu haijajitosheleza kwa kuwa na wachezaji lukuki wenye vipaji vya kutosha, bado wachezaji wa Kitanzania wanahitaji kunolewa na makocha wa kigeni.

Huwa nashangaa sana ninapomsikia Wallace Karia kuwakataa makocha wa kigeni wakati Simba na Yanga zenyewe zinapata mafanikio kwa sababu ya kunolewa na makocha wa kigeni, mbali na makocha wa kigeni, Simba na Yanga zinanufaika na wachezaji wa kigeni.

Kufungwa na Morocco ni kama tumependa wenyewe, hakukuwa na mkakati wowote kuona nchi inafuzu fainali za kombe la dunia wala kuona tunaibuka na ushindi, nyakati kadhaa zilizopita Taifa Stars iliweza kupambana na vigogo kama Morocco.

Tuliwahi kuifunga Morocco, ingawa Morocco ya leo si Ile ya wakati ule, lakini Stars ya leo imeachwa mbali sana na Stars zilizopita, TFF naona wameelekeza nguvu zake kwenye soka la vilabu na si timu ya taifa, Taifa Stars.

ALAMSIKI