MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo haitaki kufanya makosa kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Bigman.
-
Simba, inayonolewa na Kocha Fadlu Davids, itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaochezwa Alhamisi, Machi 27, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
-
Ahmed amesema licha ya Bigman kuwa timu inayoshiriki Ligi ya Championship, jina lake linatisha, na Simba inaheshimu historia ya timu kama hizo ambazo zimekuwa zikiwasumbua katika mashindano ya ndani kwa miaka ya nyuma.
-
“Tunakumbuka timu za aina hii zimekuwa na historia mbaya kwetu, kwa hiyo ni lazima tufanye vizuri. Tumekuwa na wiki mbili za maandalizi kwa wachezaji ambao hawako kwenye majukumu ya timu za taifa,” alisema Ahmed.
-
Kwa mujibu wa Ahmed, Simba ilitumia wikiendi iliyopita kucheza mechi za mazoezi kama sehemu ya maandalizi yao kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
-
“Kocha Fadlu aliona ni vyema kupata mechi ya kirafiki ndani ya wiki hii ili kupima utimamu wa kimwili wa nyota wake na kuongeza ushindani ndani ya kikosi,” aliongeza.