Mshambuliaji wa zamani wa Simba Moses Phiri anayekipiga kwa sasa Power Dynamos ya Zambia amekiangalia kikosi cha sasa wa Wekundu hao chini ya kocha Fadlu Davids na kusema anaiona kabisa ikifika mbali katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, iwapo itaamua kukaza buti.
Raia huyo wa Zambia aliyeichezea Simba kwa misimu miwili kabla ya kuondoka dirisha dogo la msimu uliopita, Alisema endapo wachezaji wakiamua kufanya muendelezo wa kiwango walichokionyesha hadi kutinga robo fainali, inaweza kuwafikisha hata fainali.
"Nimeifuatilia Simba katika mechi zao za CAF, imeonyesha kiwango na ukomavu kwa wachezaji kuamua matokeo, kadri wanavyopiga hatua ndivyo ushindani unavyozidi kuongezeka, hivyo ni kazi kwa wachezaji kuongeza bidii na wawe tayari kujitoa kwa ajili ya timu," alisema Phiri na kuongeza;
"Simba ni kati ya klabu kubwa Afrika, ndiyo maana kwa sasa inaongoza kundi lake A kwa pointi 13, hilo linaonyesha hakuna kinachoshindika endapo viongozi, makocha na wachezaji wakiamua kuweka mikakati madhubuti ya kufika fainali."