Elie Mpanzu na Joshua Mutale ni wale wale

Na Prince Hoza

NI mapacha wasiofanana naweza kusema, lakini ni ndugu moja wa familia moja, Joshua Mutale ni mchezaji wa Simba SC sawa na Elie Mpanzu.

Mutale alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu na Mpanzu amesajiliwa na Simba katikati ya msimu huu kwenye dirisha dogo la Januari mwaka huu.

Ujio wa Mpanzu una shabaha kubwa wengi wakiamini mchezaji huyo atakuwa mwarobaini wa Wekundu hao wa Msimbazi, ujio wa Mpanzu unamatarajio makubwa kwa Wanasimba wengi ulimwenguni.

Ikumbukwe Simba iliamua kufanya usajili huo wa Mpanzu baada ya kuona Joshua Mutale kushindwa kuingia kwenye mfumo sawa sawa, mchezaji huyo hakuwa kwenye ubora kama alivyotarajiwa mwanzo.

Kufeli kwa Mutale aliyesajiliwa kutoka timu ya Power Dynamos ya Zambia, kumewashangaza wengi isitoshe alikuwa kwenye ubora, mchezaji huyo akiwa Dynamos alikuwa tegemeo lao na katika Ligi ya Zambia kwa ujumla.

Wazambia hawaamini kama mchezaji huyo amefeli ndani ya Simba na kuna watu wanaamini kwamba amerogwa, lakini tusioamini ushirikina kwenye soka, tunaamini kwamba mchezaji huyo amezidiwa.

Ikumbukwe Simba iliwahi kukutana na Dynamos msimu uliopita katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika raundi ya kwanza ya michuano hiyo na katika mchezo waliokutana walitoka sare ya mabao 2-2.

Mchezo wa kwanza ulifanyika Zambia ambapo Mutale alionesha kiwango kikubwa na ndipo maskauti wa Simba walipomuona, ingawa timu hizo zilirudiana jijini Dar es Salaam na kutoka sare ya kufungana bao 1-1, Mutale tena alicheza vizuri.

Simba na Mutale waliingia makubaliano kutokana na pafomansi yake akiwa Dynamos, ndani ya Simba ilionekana wazi anakwenda kuchukua nafasi ya Willy Esomba Onana ambaye uchezaji wake haukuwa mkubwa.

Pia Mutale ambaye anacheza vizuri zaidi upande wa kulia, angemweka benchi Kibu Denis ambaye alikuwa anachezeshwa kama winga wa kulia, lakini alipoingia ndani ya kikosi cha Simba chini ya kocha Fadlu Davids, alicheza namba saba na Kibu alihamishwa upande wa kushoto.

Mategemeo hayakuwa mazuri, kiwango cha Mutale kila kukicha kinazidi kuporomoka na baadaye kuonekana mchezaji wa hovyo na anapigiwa hesabu za kutolewa kwa mkopo.

Kuna tetesi kwamba Mutale anarudishwa Dynamos baada ya kushindwa kuwaridhisha Wanasimba, wakati Mutale akiwa si lolote si chochote, uongozi wa klabu hiyo chini ya bilionea Mohamed Dewji "MO", ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo ikaamua kumsajili Elie Mpanzu.

Mpanzu ni kiungo mshambuliaji machachari ambaye alikuwa anaichezea kwa mafanikio timu ya AS Vita Club ya DR Congo, lakini mchezaji huyo alitimkia Ubelgiji kufanya majaribio katika klabu ya KRC Genk.

Mpanzu hakuwa na mpango wa kuja kucheza Afrika mashariki na mahesabu yake ni kucheza barani Ulaya, hata hivyo Mpanzu alijiunga na Simba baada ya dili lake la kucheza Ulaya kufeli na ikabidi achelewe kuchezea Simba mpaka dirisha lililofunguliwa.

Mashabiki wa Simba walikuwa wanampigia hesabu nyingi wakiamini kwamba yeye ni mchezaji mkubwa kuliko wengine, Mpanzu alianza kuonekana ndani ya uwanja akiichezea Simba kwenye mchezo wa kwanza na alicheza vizuri.

Lakini waliomtazama walimuona ni sawa na Joshua Mutale, wanafanana ni kama ndugu, NI mapacha ambao hawatokani na tumbo moja, kiwango cha Mutale ni sawa na cha Mpanzu, kikubwa kinachokwenda kumponza ni kucheza na jukwaa.

Sio Mutale peke yake anayependa kucheza na jukwaa, hata Onana naye alipenda kucheza na jukwaa sawa na Mpanzu, ipo siku mchezaji huyo ataangukia pale pale kwa Mutale ba baadaye Simba itamtoa kwa mkopo ama kumuacha moja kwa moja.

ALAMSIKI


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA