Ujio wa kipa mpya kutoka Guinea, Moussa Camara 'Spider' umemfanya winga wa Simba, Willy Onana kung'oka Msimbazi baada ya taarifa kuvuja kuwa yeye ndiye anayempisha kipa huyo aliyetua kuziba nafasi ya Ayoub Lakred aliyeumia kambini Misri.
Usajili wa Camara ni wa dharura kutokana na kuumia kwa Ayoub Lekred, ambaye alionekana tegemeo ndani ya kikosi hicho, hivyo ujio wake ataongeza nguvu dhidi ya makipa wenzake Hussein Abel na Ally Salim.
Katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo, yaliyofanyika leo Ijumaa Agosti 2, 2024, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Onana hakuwa sehemu ya kikosi na taarifa za ndani zinaeleza kashapata timu huko Qatar anayoweza kujiunga nayo wakati wowote.
Simba ilimsajili Onana, msimu uliopita kutoka Rayon Sports ya Rwanda akiwa mchezaji bora wa ligi kuu nchini humo (MVP) lakini ameshindwa kuwika huku akikumbukwa kwa mabao mawili aliyofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC.
