Na Fazila Lyimo
Hatimaye memba wa lililokuwa kundi la muziki wa kizazi kipya la Mambo Poa, Rashid Mustapha "Spider" amewajibu baadhi ya mashabiki wa kundi hilo kwamba yeye ahusiki na haki za waliokuwa wanamuziki wenzake wa kundi hilo ambao sasa ni marehemu.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari kupitia kipindi chake kinachorushwa mchana, alisema yeye asimamii kazi za wasanii hao wenzake ambao kwa sasa wametangulia mbele yaki.
Spider aliwataja wenzake hao John Mjema na Steve 2k ambao wameaga dunia lakini walifanikiwa kuachia nyimbo mbalimbali ambazo zilitikisa.
Spider amedai kwamba kwa bahati mbaya kazi zao hazijawekwa kwenye mitandao hivyo ni ngumu yeye kuzisimamia, hata hivyo Spider amedai kuwa John Mjema na Steve 2k kila mmoja anawakilishwa na ndugu zake hivyo itakuwa ngumu kwa yeye kusimamia kazi zao.
Hivi karibuni baadhi ya mashabiki wa kundi hilo walimjia juu Spider wakidai kwamba anahusika kutafuna mapato ya Steve 2k na Mjema kwakuwa wenzake hao hawapo duniani, jambo ambalo Spider ameweka wazi kwamba yeye ahusiki kabisa.
Kundi la Mambo Poa lililokuwa na nyota hao watatu lilifanikiwa kupata umaarufu nchini kutokana na wimbo wake uitwao 'Mimi sio mwizi' na nyingine Spea tairi.
