Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Kispoti

Musonye na CECAFA yenu mnaishi dunia gani?

Na Prince Hoza

MICHUANO ya Klabu bingwa Afrika mashariki na kati maarufu kombe la Kagame inatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu hapa nchini na jumla ya timu 12 zimepangwa katika makundi matatu ambapo timu nane zitavuka hadi robo fainali, michuano hiyo itapigwa katika viwanja viwili tofauti, Uwanja wa Taifa na Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Katibu mkuu wa kudumu wa Baraza la vyama vya soka Afrika mashariki Nicholaus Musonye amesema michuano ya Klabu bingwa Afrika mashariki na kati maarufu kombe la Kagame itafanyika Tanzania Bara na viwanja viwili vitatumika, Musonye alianza kutambulisha mchezo kati ya Simba Sc na Yanga Sc ambao ni mahasimu wa soka la Tanzania kwamba zitaumana Julai 5.

Musonye alisema Simba na Yanga zimepangwa kundi C, aidha Musonye aliweka wazi makundi yote matatu ambapo kila kundi lilikuwa na timu nne, Tanzania Bara inawakilishwa na timu tatu ambazo ni Yanga Sc, Simba Sc na Azam Fc, Musonye amedai Yanga imeingia katika michuano hiyo ikiwa kama bingwa wa mwaka jana na Azam Fc wameingia kama mabingwa watetezi huku Simba ikiombewa nafasi kwakuwa Bara ni waandaaji.

Akitaja makundi hayo, Musonye alisema kundi A lina timu za Azam Fc ya Tanzania Bara, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator ya Sudan, wakati kundi B lina timu za Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludik ya Burundi na Ports Fc ya Djibout.

Wakati kundi C lilikuwa na timu za Yanga Sc, Simba Sc za Tanzania Bara, Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia, michuano hiyo haipo kwenye kalenda ya FIFA, CAF wala TFF na imekuwa ikifanyika kwa kuzuka tu.

Mara ya mwisho kufanyika Kagame Cup ilikuwa mwaka 2016 ikifanyika Dar es Salaam ambapo timu ya Azam Fc ya Tanzania Bara ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Gor Mahia mabao 2-0, baada ya hapo haikufanyika tena, na kufuatia Musonye kuanika makundi yote, Klabu ya Yanga ikaliandikia barua Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania Bara (TFF) ikitaka kujitoa.

Yanga Sc ilitoa sababu za kutaka kujitoa lakini kubwa ni kutokuwa na wachezaji wa uhakika kwani wachezaji saba tu wa kikosi hicho ndio wenye mikataba na waliobaki mikataba yao imekwisha hivyo isingewekana kuwapata na kuwapeleka kambini kujiandaa na michuano hiyo, lakini sababu ya pili wamedai wanajiandaa na michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo timu hiyo itaumana na Gor Mahia ya Kenya mapema mwezi ujao.

Katibu mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa alisema kwamba wamewapa likizo wachezaji kusudi wakirejea wataingia kambini kujiandaa na mchezo wao na Gor Mahia utakaofanyika Kenya, kujitoa kwa Yanga kulizua utata kwani ilipangwa pamoja na mtani wake Simba na Julai 5 mwaka huu zingeumana.

Baada ya Yanga kuandika barua ya kuomba kujitoa, Rais wa TFF Wallace Karia aliwapa masaa 48 Yanga kutengua maamuzi hayo na kushiriki Kagame Cup, Lakini Yanga wakakomaa na msimamo wao na hatimaye CECAFA ikaridhia Yanga kujitoa katika mashindano hayo makubwa katika ukanda huu.

Baada ya Yanga kujitoa, timu ya Saint George ya Ethiopia nayo ikajitoa katika mashindano hayo yaliyokosa mdhamini hadi sasa na vilevile yamepungua msisimko wake, CECAFA ikaridhia kujitoa kwa Saint George na tayari imeshaziongezea timu mbili nyingine ambazo zimeziba nafasi za Yanga na Saint George, Singida United na APR sasa zimechukua nafasi hizo hivyo michuano itaenda kama kawaida, wakati miamba hiyo ya Ethiopia na Tanzania Bara ikijitoa, Klabu ya Gor Mahia ya Kenya nayo imesema kwamba italeta kikosi chake cha pili kwenye michuano hiyo ili kuwapumzisha nyota wake akina Meddie Kagere, Jacques Tuyisenge, George Walusimbi na wengineo kujiandaa vema na michuano ya Afrika.

Gor Mahia itaumana na Yanga katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika Julai 16 au 18 mwaka huu, kufuatia Gor Mahia kutangaza kuleta "Yosso", mabingwa wa Bara Simba Sc nao wametangaza kutumia kikosi B kikiwa na mchanganyiko wa baadhi ya nyota wake waliokuwa hawapati nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara, huku ikiwapumzisha mastaa wake.

Simba imesema haitamtumia kipa wake mahiri Aishi Manula katika michuano hiyo pia kiungo wake Jonas Mkude, kwa maana hiyo wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi ya kucheza hasa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambapo timu hiyo ilichukua ubingwa.

Michuano ya Kagame kimuonekano inazidi kupungua mvuto, na kwa bahati mbaya waandaaji wa michuano hiyo CECAFA pamoja na katibu mkuu wake Nicholaus Musonye sijui wanaishi ulimwengu gani kwani wameipeleka michuano yao sambamba na kombe la dunia.

Nani asiyejua utamu wa kombe la dunia, na michuano ya mwaka huu inafanyika nchini Urusi na tayari uhondo umeshaanza ambapo miamba yote duniani ipo Urusi, mechi zinapigwa mchana, jioni mpaka usiku, hivi unadhani nani ataenda kutazama kombe la Kagame.

Kama malengo yao yalikuwa kukusanya pesa za viingilio basi wamegonga mwamba, Yanga wamejitoa na Simba watatumia wavhezaji wa akiba huku Gor Mahia ikileta yosso, nani ataenda kutazama michuano hiyo, tusidanganyane hapa Musonye na CECAFA yake sijui wanaishi dunia gani!

Nawauliza hivyo kwa sababu hawajui heshima ya kombe la dunia, michuano yote ulimwenguni imesimama kupisha kombe la dunia, inakuwaje Musonye anaamka usingizini na kuanzisha mashindano ambayo nahisi yatapotea kabisa kwani hakuna mtu atakayejali kama kuna michuano hiyo mbele ya kombe la dunia. Kuna wakati Musonye anajiona anaishi katika dunia ya peke yake

Alamsiki

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

Ngao ya Jamii sasa ni Simba na Yanga

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limebadilisha kanuni za mashindano za Ngao ya Jamii kutoka timu nne na sasa utaratibu utakuwa kama zamani. Bingwa wa Ligi Kuu bara atacheza na mshindi wa kombe la CRDB Cup "CRDB Federation Cup, na endapo kama bingwa wa ligi na CRDB atakuwa ni mmoja basi mshindi wa pili kwenye Ligi Kuu ya NBC atacheza mchezo wa ufunguzi wa ligi yaani Ngao ya Jamii.  Hivyo ni rasmi ufunguzi wa wa ligi kuu mchezo  wa "Ngao ya Jamii msimu huu 2025-2026 ni Yanga na Simba watakutana.

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...