Wanachama Simba sasa wakataa 'Mbumbumbu' kuwania Urais, Ujumbe

Na Saida Salum. Dar es Salaam

Mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika hii leo katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Ocean Road ulioudhuriwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dr Harrison Mwakyembe umepitisha katiba mpya ya kuelekea kwenye kampuni ambapo sasa Simba itaendeshwa kwa Hisa.

Katika mkutano huo ulioitishwa na kaimu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah "Try Again", na kuudhuriwa na zaidi ya wanachama 1000 ulipitisha mpango wa kuuza Hisa asilimia 49 kwa mwekezaji na asilimia 51 kubaki kwa wanachama kama ambavyo serikali imezitaka klabu za wanachama kufanya hivyo.

Tayari mfanyabiashara, Mohamed 'Mo' Dewji ambaye alikuwa mwanachama pekee wa klabu hiyo kujitokeza na kutaka kununua Hisa asilimia 51 kwa kumwaga Bilioni 20 alisharidhia kununua Hisa asilimia 49 hivyo leo ilikuwa kazi ndogo tu kurekebisha baadhi ya vifungu.

Wanachama haowalikubaliana Simba ijiendeshe kisasa na huenda msimu ujao ikatumia uwanja wake wenyewe kuchezea mechi zake za Ligi Kuu Bara na mechi za kirafiki, pia wanachama wameamua kuwa hawataki tena mbumbumbu kuwania vyeo vya ngazi ya juu kwani kuanzia Rais (Mwenyekiti wa Bodi) na wajumbe wake wanne wawe na shahada.

Pia nafasi ya katibu mkuu nayo imefutwa rasmi na sasa kutakuwa na mkurugenzi mtendaji ambaye atawajibika kama katibu, aidha mwanamke mmoja atachaguliwa kuwa mjumbe ili kuweka uwiano sawa

Wanachama wa klabu Simba walikutana leo kujadili mambo yao