Na Salum Fikiri Jr. Dar es Salaam
Mabingwa wa soka nchini Simba SC walipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ilipokea kichapo hicho mbele ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli siku ya Jumamosi ya Mei 19 mwaka huu, Simba ilikabidhiwa ubingwa wake ilioutwaa Mei 10 mwaka huu na hasa baada ya mahasimu wao Yanga kulala mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Katika mchezo kati ya Simba na Kagera ulioudhuriwa na Rais Magufuli, Simba ilijikuta ikibanwa na kuchapwa bao hilo moja lililofungwa na Christopher Edward ambaye alilelewa na Simba.
Wafuatao ni nyota wanne ambao waliikatia umeme Simba SC mbele ya Rais Magufuli
1. Juma Kaseja
Kipa mkongwe aliyepata kuzichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, kipa huyo alikuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Simba ambao walishindwa kumfunga, sifa yake kubwa kwenye mchezo huo ni pale alipoweza kuokoa penalti iliyopigwa na Emmanuel Okwi.
2. Juma Nyoso
Naye amewahi kuichezea Simba pamoja na Coastal Union, alikuwa kizingiti kikubwa na kuweza kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Simba ambao wanasifika kwa kucheka na nyavu, Nyoso alifanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi yote ya Simba.
3. George Kavila
Kiungo huyu mkongwe aliingia kipindi cha pili lakini alionyesha kuwadhibiti Simba na kufanya matokeo ya mchezo kuwa hivyo, Kavila hakuwa na masihara mbele ya Rais Magufuli kwani kila mpira aliouona mbele yake aliuondosha.
4. Christopher Edward
Mfungaji wa goli pekee la ushindi lililomsababishia Rais Magufuli apeleke sifa kwa Kagera Sugar badala ya Simba ambao ndio mabingwa wa soka nchini, Edward alifunga bao la ushindi.
5. Peter Mwalyanzi
Naweza kusema huyu ndiye mkata umeme kwa viungo wa Simba ambao haakufua dafu kwake mpaka Rais Magufuli akatamka maneno kuwa kwa Simba hii kimataifa bado, Mwalyanzi aliwahi kuichezea Simba akitokea Mbeya City ya jijini Mbeya