Ngasa kurejea Yanga kwa mara ya tatu

Na Saida Salum. Dar es Salaam

Klabu ya Yanga iko mbioni kumalizana na kiungo mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngasa wa Ndanda Fc ya Mtwara kwa mkataba wa mwaka mmoja imebainika, taarifa zilizosambaa jana zinasema tayari mchezaji huyo ameshazungumza na viongozi wa klabu hiyo na muda wowote kuanzia sasa anaweza kumwaga wino.

Ngasa amecheza vizuri akiwa na Ndanda Fc na kuipigania timu hiyo kusalia Ligi Kuu Bara mpaka mabosi wa Yanga kuvutiwa naye na kuamua kumrejesha tena mitaa ya Jangwani kwa mara ya tatu, Ngasa alijiunga Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2006 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba kabla hajanunuliwa na Azam Fc kwa usajili uliovunja rekodi mwaka 2010, nyota huyo akidumu Azam Fc na baadaye akajiunga na Simba kabla hajarejea Yanga kwa mara pili.

Ngasa hakudumu sana Jangwani kwani akajiunga na Free State Stars ya Afrika Kusini ambako nako hakudumu akavunja mkataba na kujiunga na Fanja ya Oman, pia hakudumu akarejea nyumbani Tanzania na kujiunga na Mbeya City aliyodumu nayo kwa nusu msimu kabla hajajiunga na Ndanda Fc, Akiwa na Ndanda, Ngasa ameonyesha kiwango kizuri ambapo Yanga kwa mara ya tatu wanaamua kumrejesha tena kikosini, mchezaji huyo juzi alionekana mitaa ya klabu hiyo Jangwani akisalimiana na wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo.

Jana uongozi wa Yanga ulipinga vikali usajili wa Ngasa na ikidai mchezaji huyo alienda Jangwani kuwasalimia tu na hawana mpango wa kumrejesha, lakini taarifa mpya zinasema Ngasa ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Yanga watakaoshiriki katika mashindano yajayo ikiwemo kombe la Shirikisho barani Afrika

Mbali na Ngasa, Yanga pia inatajwa kutaka kumsainisha mshambuliaji wa Simba Mohamed Ibrahim "Mo" na kiungo wa Mbao Fc ya Mwanza, Habib Kiyombo

Mrishp Ngasa kurejea tena Yanga