Majina ya wachezaji 30 watakaowania tuzo za VPL hawa hapa

Na Asher Maliyaga. Dar es Salaam

Shirikisho la mpira wa miguu nchini, TFF limetangaza jumla ya wachezaji 30 wanaocheza Ligi Kuu Bara hapa nchini watawania tuzo mbalimbali za wachezaji bora kwa mwaka huu inayotarajiwa kutolewa Juni 23 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa Shirikisho hilo, Clifford Ndimbo imesema kwamba kufanyika kwa tuzo ni utaratibu ambao Shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini, TFF limejiwekea kila mwaka baada ya kumalizika Ligi Kuu.

Tuzo hizo zitatolewa chini ya wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi, Vodacom na Azam Tv huku wakiongezeka wadhamini wengine ambao ni benki ya KCB na Primier Bet, alisema Ndimbo. Aidha Ndimbo amedai TFF imefuta tuzo ya mchezaji bora wa kigeni.

Licha ya kufutwa tuzo hiyo, Ndimbo amesema kutakuwa na tuzo mbalimbali za wachezaji bora, tuzo zirakazotolewa ni Timu yenye nidhamu, Mchezaji bora chini ya umri wa miaka 20, (Ismail Khalfan), Mchezaji bora chipukizi, Mwamuzi bora, Kipa bora, Kocha bora, Bao bora, Kikosi bora cha wachezaji 11 wa Ligi Kuu na mchezaji wa heshima.

Kamati ya tuzo imetaja majina ya wachezaji hao 30 watakaoshindanishwa kwenye tuzo hizo ambao ni Habibu Kiyombo (Mbao Fc), Khamis Mcha (Ruvu Shooting), Yahya Zayed, Razack Abalora, Bruce Kangwa, Himid Mao wote wa Azam Fc, Awesu Awesu (Mwadui Fc), Adam Salamba (Lipuli) Mohamed Rashid (Prisons), Shafik Batambuze, Mudathir Yahya, Tafadzwa Kutinyu wote wa Singida United.

Wengine ni Marcel Kaheza (Majimaji), Ditram Nchimbi (Njombe Mji), Eliud Ambokile (Mbeya City), Shaaban Nditi, Hassan Dilunga wa Mtibwa Sugar, Ibrahim Ajib, Gardiel Michael, Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Kelvin Yondan wa Yanga SC, Aishi Manula, Emmanuel Okwi, John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya na Asante Kwasi wote wa Simba ambayo jumla imetoa wachezaji saba ikifuatiwa na Yanga na Azam kila moja ikitoa watano

Tuzo za wachezaji bora VPL zitatolewa Juni 23 mwaka huu