Kispoti

Alphonce Modest anahitaji msaada wa wadau wa soka na serikali

Na Prince Hoza

RAIS wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli aliudhuria kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa soka kati ya Simba SC Kagera Sugar wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Magufuli alikuwa mgeni wa heshima na aliweza kuikabadhi kikombe cha ubingwa wa Ligi Kuu Simba SC na vilevile aliikabidhi kikombe timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ambayo ilifanikiwa kubeba kombe la mataifa Afrika mashariki na kati yaliyofanyika nchini Kenya.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini, TFF, Wallace Karia alimuomba Rais Magufuli awe mgeni wa heshima katika mchezo huo ili kukabidhi ubingwa kwa Simba SC na Serengeti Boys ambao ni mabingwa wa CECAFA. Hata hivyo kaimu katibu mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alitoa ufafanuzi kuhusu TFF kumuomba Magufuli awe mgeni wa heshima katika mchezo huo.

Kidao alisema kuhudhuria kwa mheshimiwa Rais Magufuli na kukabidhi ubingwa wa Ligi Kuu Bara kunaongeza thamani ya Ligi hiyo na kuwavutia wadau wengine na huenda kukaongezeka kwa wadhamini.

Lakini hayo yametokea huku mlinzi wa zamani wa Tanzania aliyepata kuwika katika vilabu vya Pamba FC ya Mwanza, Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam, pia akitamba katika timu zote za taifa, Taifa Stars na ile ya Tanzania Bara, Alphonce Modest akiteseka.

Modest aliibuka mjini Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Mtibwa Sugar na Lipuli FC ya Iringa uliofanyika kwenye uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Modest akikokotwa katika kiti chake cha mataili na mkewe akisaidiwa pia na kocha wa Lipuli, Seleman Matola aliingia uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo akiwa kama mgeni wa heshima.

Inasikitisha sana kumuona staa huyo wa zamani aliyeiletea heshima kubwa nchi akitaabika, maisha anayoishi mkongwe huyo yanasikitisha, watu wa karibu wa Modest wanasema anahitaji msaada mkubwa tena ikiwezekana kutoka kwa wadau wa mchezo huo ikiwemo serikali.

Leo hii ninatumia fulsa hii kumuomba mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli kumsaidia beki huyo, ninaamini Rais Magufuli anayo dhamira ya dhati ya kuweza kuusaidia mchezo wa soka na ndio maana akaridhia kuwa mgeni wa heshima, Simba SC na Kagera Sugar.

Nina matumaini kabisa Rais Magufuli ni mpenda michezo hasa soka hivyo anapozipata taarifa hizi za huzuni kwa vyovyote anaweza kushituka, Alphonce Modest aliinukia katika timu ya Pamba FC ya Mwanza miaka ya mwanzoni na 90 akajituma mpaka akasajiliwa na Simba SC ya jijini Dar es Salaam.

Itakumbukwa kuwa mwaka 1998 Yanga SC ilituma maombi kwa watani zao Simba ikitaka iazimwe nyota wawili ambao ni beki wa kushoto wakati huo Alphonce Modest na mshambuliaji, Monja Liseki, Yanga ilifikia maamuzi ya kuwaomba nyota hao baada ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika, iliyoshirikisha timu nane.

Uongozi wa Simba bila kinyongo ukakubali kuwaruhusu nyota hao wawili na wskaanza kuitumikia Yanga katika michuano hiyo mikubwa kabisa Afrika kwa upande wa vilabu, leo hii Modest anakokotwa kwenye kiti maalum na mkewe wakati alikuwa akikokota yeye mpira.

Modest anaendeshaje maisha yake na famiia yake! anawezaje kujikimu! kwa vyovyote anaishi kwa matumaini, unadhani mateso anayopitia yanaleta picha gani kwa chipukizi kama Gardiel Michael, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Jamal Mwambeleko na wengineo.

Mchezo wa soka utaonekana hatari zaidi na sidhani kana kuna mchezaji atatamani kuendelea nao, maisha ya wachezaji wetu yanasikitisha sana, tumepoteza wachezaji wengi mashuhuri kwa maradhi huku wakiachwa ilihali walihitaji msaada, Athuman Juma Chama "Jogoo" alitaabika na maradhi yake mpaka akatutoka, Christopher Alex Masawe naye alipoteza maisha bila msaada wowote akiugua kifua kikuu, Alex alihitaji msaada lakini akaachwa, bado Jellah Mtagwa anaishi kwa taabu na maradhi yake.

Wadau wa soka sidhani kama wanawakumbuka nyota wao waliopata kutamba katika vilabu vyao na timu yao ya taifa, nimeona bora nimuombe mheshimiwa Rais Magufuli ili amsaidie Alphonce Modest ambaye anahitaji msaada wa hali na mali. Siyo Modest peke yake tu ndiye anayehitaji msaada na wengineo ambao waliiletea heshima kubwa nchi, Modest alisaidia kupatikana kwa kombe la Castle Chalenge Cup, ambapo timu ya taifa, Taifa Stars ililitwaa,watu wa Simba nao mnahitajika kumsaidia shujaa huyu.

Pia watu wa Yanga nao mnapaswa kumkumbuka shujaa huyu, Modest anahitaji msaada akiwa anajiona, anahitaji ashuhudie kama alivyoweza kuwafanya mpate furaha. Msisubiri atutoke ndio muoneshe ufahari kushiriki mazishi yake kama ilivyozoeleka na ndiyo maana nimemuomba Rais Magufuli nikiamini Modest atapatiwa msaada haraka.

Ninachompendea Rais wetu ni sikivu sana na muelewa pia ni mnyenyekevu kwa watu wanyonge kama Modest, Rais Magufuli alijitokeza kumsaidia muigizaji Wastara Juma Sajuk aliyehitaji msaada wa kimatibabu ya mgongo yakafanyikie nchini India, Rais Magufuli alijitokeza kumsaidia, ila tusimwachie Rais peke yake , nasi tunahitajika kumuunga mkono katika kusaidia watu walioipigania nchi yetu

Alamsiki

NAWATAKIA RAMADHAN KARIM