KIPA WA DRC ALIYETUNGULIWA NA KICHUYA ATUA YANGA

Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam

Kocha mpya wa Yanga SC, Mkongoman, Mwinyi Zahera anatarajia kumshusha katika kikosi hicho kipa wa kimataifa wa DRC, Vumi Ley Matampi ambaye ni kipa wa kwanza wa kikosi cha timu ya taifa ya DRC, The Leopords ambayo ilifungwa mabao 2-0 na timu ya taifa, Taifa Stars Machi 27 mwaka huu.

Katika mchezo huo wa kirafiki uliotambuliwa na FIFA, kipa huyo alikubali kutunguliwa mabao mawili na winga, Shiza Kichuya ambaye pia ni mchezaji wa Simba SC ya Tanzania Bara ambao ni mahasimu wa Simba.

Tayari wachezaji wawili nao kutoka DRC wameshawasili na wanatazamiwa kuanza mazoezi Alhamisi na wachezaji hao watakuwepo katika kikosi kitakachoenda nchini Kenya kushiriki kombe la Sportpesa, wachezaji waliotua ni Alain Mulumba ambaye ni winga wa kulia anayekipiga DC Motema Pembe na Cedrick Kabale kiungo mchezeshaji anayekipiga timu ya Don Bosco zote za huko huko DRC.

Nyota hao watajaribiwa kupitia michuano hiyo na kama watafanya vizuri watasajiliwa moja kwa moja na kushiriki katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga itaanza kucheza mechi yake ya kwanza ya kombe la Sportpesa dhidi ya Tusker ya Kenya Juni 6 mwaka huu

Kipa wa DRC, Vumi Ley Matimpa amejiunga na Yanga