KAMUSOKO AITOLEA GUNDU YANGA, IKIICHAPA MBAO FC

Na Ikram Khamees. Dar es Salaam

Kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko jioni ya leo ameifutia aibu klabu yake ya Yanga baada ya kuichapa Mbao FC bao 1-0 mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bao hilo lilipatikana kunako dakika ya 26 kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa adhabu ndogo uliompita kipa wa timu hiyo ambaye alishindwa kuwapanga mabeki wake vizuri, kwa ushindi huo Yanga inafikisha pointi 51 na ikiwa imecheza mechi 28 lakini bado wanaendelea kukaa nafasi ya tatu.

Tayari Yanga imeshavuliwa ubingwa wa Bara na mahasimu wao Simba SC waliofikisha pointi 68 wakiwa na mechi moja mkononi, Yanga itashuka tena uwanjani siku ya Ijumaa ikicheza na Ruvu Shooting kisha Jumatatu ijayo itaumana na Azam FC mechi ya mwisho ya kufunga msimu.

Katika mchezo wa leo Yanga ilionekana kulishambulia zaidi lango la Mbao na kama si washambuliaji wake kutokuwa makini huenda wangeibuka na ushindi mnono

Thabani Kamusoko (Mwenye jezi ya kijanj) ameifungia Yanga goli la ushindi