Baada ya kupitisha katiba, Simba kumjadili Mfaransa wao

Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam

Baada ya jana wanachama wa klabu ya Simba kuipitisha katiba yao kwa kishindo na sasa kuingia rasmi katika mtindo wa kampuni ya kuuz Hisa, Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo inatarajia kukutana hivi karibuni kumjadili kocha wao mkuu Mfaransa, Pierre Lechantre.

Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika siku za hivi karibuni ikiwa ni siku chache tangu Simba ikabidhwe ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli Jumamosi iliyopita katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Taarifa ambazo Mambo Uwanjani imezipata zinasema kuwa kamati ya utendaji inakutana ili kumjadili kocha huyo ambaye ameiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara baada ya miaka mitano ikisota bila mafanikio, Lechantre alisaini mkataba wa miezi sita ambao unamalizika mwishoni mwa msimu hivyo uongozi unaazimia kumuongeza mkataba mpya.

Licha ya Simba kufungwa bao 1-0 mbele ya Rais Magufuli, lakini kocha huyo ameonesha uwezo mkubwa wa kuiongoza timu hiyo ingawa pia kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya mashabiki wakimtaka abadilike na mfumo wake kwani kwa sasa Simba imeanza kupungua makali tofauti na alivyoikuta ikiwa chini ya kaimu kocha, Mrundi, Masoud Djuma Irambona

Kocha wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre anajadiliwa