Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Kispoti: HAKUNA USHIRIKINA KWENYE SOKA

Na Prince Hoza. Dar es Salaam

HATIMAYE ubishi wa mashabiki wa soka umemalizwa Jumapili ya Aprili 29, 2018 wakati Simba Sc ilipoizamisha Yanga Sc bao 1-0 mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Goli pekee la Simba lilifungwa na Erasto Nyoni katika dakika ya 37 na ushindi huo moja kwa moja unawafanya wafikishe pointi 62 ikibakiza pointi 6 tu ili waweze kutwaa ubingwa wa bara kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.

Pia Jumapili ilikuwa siku nzuri kwa mashabiki wa Tanzania hasa baada ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Burundi kwa kuilaza Somalia mabao 2-0, shukrani ziwaendee Edson Jeremiah na Jaffari Mtoo kwa mabao yao yaliyoipa kikombe Tanzania.

Lakini mada yangu ya leo ni kuhusu Kamati ya Nidhamu na Maadili ya Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania, Tff kutoa maamuzi yake juu ya uendeshaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kamati hiyo iliweza kutoa adhabu kwa vilabu ambavyo vilifanya makosa pamoja na kuwafungia wachezaji na makocha walioonyesha utovu wa nidhamu, lakini Tff licha ya kutoa adhabu, iliingiza masuala ya ushirikina jambo ambalo lilizua mshangao kwa baadhi ya watu.

Tff ni chombo kikuu kinachosimamia soka hapa nchini lakini kimenishangaza pale kinapoamini vitendo vya kishirikina, kwa imani yangu mimi siwezi kuamini kabisa vitendo hivyo na hata malezi yangu niliyoyapata kutoka kwa baba na mama ingawa hawapo duniani kwa sasa hawakuwahi kuniaminisha kitu hicho.

Lakini Tff wamekuwa wa kwanza kuniaminisha jambo ambalo linazua utata, Kamati hiyo iliipiga faini klabu ya Simba kwa kitendo cha kulitupilia mbali taulo la kipa wa Njombe Mji Rajabu Mbululu wakati Simba ilipoumana na timu hiyo uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, katika mchezo huo Simba ilishinda mabao 2-0.

Mbali na kutupa taulo, Simba iliadhibiwa tena kwa madai ya wachezaji wake kutoingia katika vyumba vya kubadilishia nguo, pia kocha wa Azam Fc, Mromania, Aristica Cioaba amefungiwa mechi tatu kwa kumtusi mwamuzi, huku kiungo mshambuliaji wa Singida United, Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu kufungiwa mechi tatu baada ya kutupa kwa mashabiki glovu za kipa wa Mtibwa Sugar.

Vitendo vyote hivyo ni utovu wa nidhamu na wala si ushirikina, ninavyojua mimi ushirikina hauwezi kuonekana kwa macho kwani ni sawa na imani nyingine zilizopita ambazo hazionekani waziwazi, kuamini ushirikina moja kwa moja ni upotofu wa kifikra.

Shirikisho la mpira wa miguu nchini, Tff mnapaswa kuzionya klabu ama wachezaji kwa kosa la utovu wa nidhamu pasipo kuhusisha na imani hizo potofu, nilishangaa sana mashabiki wa soka hasa waliokwenda kushuhudia pambano la watani Simba na Yanga lililofanyika jana Jumapili uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuamini moja kwa moja imani za kichawi.

Kuna mashabiki nilikaa nao baada ya mpira kumalizika niliwashangaa wakihusisha njiwa waliokuwa wameshikiliwa na mashabiki wa Simba kuwa ni uchawi, njiwa anahusishwaje na uchawi wakati ni ndege kama wengine, hata wale waliokuwa na vibuyu nao wakisihusishwa na ushirikina.

Kuna wakati tunatakiwa kuenzi asili na tamaduni zetu za Kiafrika hasa kukaa na mifugo yetu ama vyakula vyetu, siamini kama ushirikina una nafasi kwenye mpira wa miguu, mchezo huo ni sayansi hivyo hauwezi kuingiliana na kitu kingine, vyombo vya habari vilivyoandika taarifa za ushirikina hasa baada ya Tff kutoa adhabu naona navyo havikufanya vizuri.

Ni aibu tena kubwa kwa Tff kutoa adhabu kisa ushirikina badala ya utovu wa nidhamu, umefika wakati sasa tuachane na mambo hayo ili kuweza kupiga hatua, wenzetu walioendelea kisoka sidhani kama wanaweza kutoa adhabu kwa klabu au mchezaji kisa ameshiriki ushirikina.

Tumeona matukio mbalimbali kwenye nchi za wenzetu hasa yanayofanana na ya hapa nyumbani lakini yanahusishwa na utovu wa nidhamu na siyo ushirikina, hakuna ushirikina kwenye mchezo wa soka, jitihada binafsi na kufuata vema maelekezo ya wataalamu yanatosha kabisa kutafuta matokeo uwanjani, kama kuna njia za mkato kusingetumika fedha nyingi kusajili na kupeleka timu kambini.

Tusipende sana kuhusisha ushirikina na utovu wa nidhamu kwani matukio hayo nayaona yakifanyika mara kwa mara lakini vyombo vya juu hasa Tff vikiyaita ni ushirikina kitu ambacho si kweli, wakati nipo mdogo niliaminishwa kuwa maeneo ya Sumbawanga, Bagamoyo na Tanga yanasifika kwa uchawi.

Lakini nikashangaa pia nikiona maeneo hayo yakishindwa kung' ara kwenye mchezo wa soka, Tanga angalau kuna timu za Coastal Union, African Sports na Mgambo JKT, lakini Bagamoyo na Sumbawanga hawana hata timu ya daraja la pili

Tuonane tena Wiki ijayo Inshallah Mungu akipenda

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...

Mabululu ni wa Simba SC

Simba wameweka donge nono kunasa saini ya mshambuliaji Agostinho Cristovan Paciencio Mabululu anayekipiga Al Tripoli ya Libya Ili ajiunge na Wekundu hao wa Msimhazi. Simba wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja na wakala wa Mabululu na mchezaji mwenyewe na wako tayari kulipa kiasi cha juu zaidi kunasa saini ya mshambuliaji huyo hatari zaidi Simba wanahitaji kumalizana na mshambuliaji huyo badala ya kumaliza fainali ya kombe la Shirikisho, tayari Crecentius Magori yuko nyuma ya mpango huo kuhakikisha Simba ijayo inatisha. Mbali na Mabululu, Simba pia inahitaji Saini ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC Feisal Salum "Feitoto" ambaye pia amewahi kuichezea Yanga SC