Na Ikram Khamees, Dar es Salaam
Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) kupitia kamati yake ya Sheria na Hadhi za wachezaji leo imepitisha usajili wa vilabu vinavyoshiriki Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL) na Ligi Daraja la kwanza (FDL) huku ikipitisha jina la beki Hassan Ramadhan Kessy kuichezea Yanga msimu huu wa 2016/17.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Richard Sinamtwa amempitisha Kessy akidai alisajiliwa kihalali na hata madai ya klabu yake ya zamani ya Simba hayaendani na usajili wake, Kessy alisota benchi kwa muda mrefu baada ya klabu yake ya zamani ya Simba kumuwekea ngumu asicheze.
Hata hivyo mchezaji huyo akaanza kucheza kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo Yanga ilikutana na Azam FC Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, na katika mchezo huo Yanga ililala kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya kumaliza dakika 90 kufungana mabao 2-2, Kessy alikosa penalti katika mchezo huo