ANAYEKUMBUKWA: HABIBU MAHADHI, MFUNGAJI BORA LIGI KUU SAFARI LAGER 1998

Na Salum Fikiri Jr, DAR ES SALAAM

ANATOKEA kwenye familia ya marehemu Omary Mahadhi bin Jabir kipa wa zamani wa African Sports, Simba SC na Taifa Stars, Habibu Mahadhi ni mtoto wa gwiji hilo la soka miaka ya 70 na 80.

Habibu alitamba na Coastal Union ya Tanga akitumia guu la kushoto na aliibuka mfungaji bora wa Ligi kuu ya Safari Lager mwaka 1998 wakati huo ikichezwa kwa hatua ya makundi.

Habibu aliyeanzia kwenye timu ya mtaani kwao Magomeni Kota ya Police Kids baadaye akajiunga na Big Bon ya Magomeni Mikumi timu aliyokaa nayo hadi aliporejea timu ya mtaani kwake ya Messina Linea.

Big Bon iliyoanzia Ligi Daraja la nne ikapanda hadi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa wa Dar es Salaam, kwa bahati mbaya timu hiyo ikavunjwa hasa baada ya aliyekuwa mfadhili wake Ahmed Bashwani kuachana na ufadhili.

Mahadhi na wenzake wakaondoka na ndipo alipojiunga na Messina, Mahadhi na nyota mwenzake George Kavila wakaenda zao Coastal Union ya Tanga na katika msimu wake wa kwanza akaibuka mfungaji bora wa ligi kuu bara.

Chakushangaza mchezaji huyo ambaye ni kaka wa Waziri Mahadhi "Mendieta" aliyepata kutamba pia na Coastal Union, Yanga na Moro Ubited pamoja na Taifa Stars alizikacha ofa za Yanga na Simba.

Mahadhi akitumia guu lake la kushoto alikataa ofa ya Yanga kisha baadaye ya Simba na kikubwa alisema timu hizo zingekuwa tayari kumpa dau kubwa angejiunga na moja wapo, Mahadhi alilamba Milioni moja ya ufungaji bora ambayo ilimsaidia kukamilisha ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam

Habibu Omari Mahadhi akiwa amejipumzisha nje ya nyumba yake