Ruka hadi kwenye maudhui makuu

KINNAH PHIRI AJA KUMRITHI MWAMBUSI MBEYA CITY

NI takribani mwezi mmoja sasa tangu aliyekuwa kocha mkuu wa Mbeya City Fc (timu ya kizazi kipya) Juma Mwambusi alipotangaza rasmi kuachana na timu hii ili kwenda kujiunga na Young African ya Dar es Salaam ambayo pia inashiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara kama ilivyo City.

Kujiunga na Yanga, safari ya Mwambusi aliyedumu ‘kikosini’ takribani miaka mitano na kupatia mafanikio makubwa, ni wazi imekuwa na baraka tele kutoka kwa uongozi, wadau na mashabiki wa hasa kwa yote aliyoyafanya ndani ya timu hii, ndiyo maana mpaka leo hajawahi kukutana na kadhia yoyote kuhusu kuondoka kwake kikosini.

Kwa wadau wa soka, kuhama kutoka timu moja kwenda nyingine kunakowakuwata wachezaji, makocha na kwa uchache viongozi ni jambo la kawaida ambalo linafanyika kwa lengo moja tu kuongeza mafanikio kwa pande zote zinazohusika, huku maslahi yakiwa ‘chagizo kuu’ kwa upande mwingine.

Safari ya kocha Mwambusi kutoka kwenye timu aliyoshiriki kuianzisha na kudumu nayo kwa miaka mitano kwenda timu nyingine hakika ni tiketi ya mwalimu mpya kuja kuliongoza bechi la ufundi la City kwa lengo la kusukuma mbele yote yaliyokwisha fanywa hapo kabla.


Kwenye hili ni bora ifahamike kuwa yapo maombi mengi ‘kupitiliza’ kutoka ndani na nje ya Tanzania yanayohitaji tiketi (nafasi) ya kuongoza benchi la ufundi la timu ya kizazi kipya huku Kinnah Phiri likiwa ndiyo jina linalotajwa sana na mashabiki wa timu hii kuwa ndiye mtu sahihi wa kuvaa viatu vya Mwambusi.

Kwa nini Kinnah Phiri..! huenda mashabiki hao wanaguswa na historia nzuri ya kocha huyu wa zamani wa Free State ya Afrika Kusini na raia wa Malawi aliyeanza kupata mafanikio ya soka akiwa mshambuliaji kwenye timu za Big Bullets ya nchini kwao pia Manzini Wanderers ya Swaziland ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kucheza michezo 30 na kufunga mabao 36 akiwa na jezi ya The Flames (timu ya taifa ya Malawi) 1974-1981.

Kutajwa sana kwa jina hili na mashabiki wa City ndiyo sababu ‘iliyomuinua kitini’ Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe, kutoka mbele ya vyombo vya habari na kuzungumza juu ya hili akisema kuwa kwenye soka kuna mambo mengi wakati mwingine linalotarajiwa hukosekana na lisilotarajiwa hutokea.

“Baada ya kuondoka Mwambusi ni wazi nafasi ikabaki wazi, binafsi nimesikia juu ya kocha Phiri kwa muda mrefu ila naomba niseme mbele yenu kuwa kwenye soka kuna mengi, huyu ni kocha mzuri mwenye sifa zote yawezekana akawa au asiwe kikubwa ni uhitaji na aina ya uhitaji wenyewe” alisema.

Tuanzie hapo,’huyu ni kocha mzuri mwenye sifa zote’ sawa kwenye mlengo upi? Hilo ni swali lingine, imani iliyopo ni kuwa anatajwa sana kwa sababu ni mmoja wa makocha wenye uwezo wa kujenga kikosi cha nguvu na ushindani kinachoweza kupambana dakika zote 90 popote kwa lengo la kutafuta matokeo.

Novemba 25,2008 jarida moja la michezo huko Afrika Kusini lilindika habari iliyobebwa na maneno ‘Malawi yarejea kwenye ramani ya soka’ hii ni kufuatia mwanzo mzuri kwenye michezo ya awali kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika ambazo zilipangwa kuchezwa baadae huko Angola.

Akiwa kiongozi wa benchi la ufundi kwenye kikosi cha Free State ya Afrika Kusini kwa misimu minne tofauti alikuwa na matokeo ya kubadili nafasi kwenye msimamo PSL,kitu muhimu ni kuwa alifanikiwa kuijenga timu hiyo kutoka timu ya kawaida kuwa ya ushindani, huyo ndiyo Kinnah Phiri mwenye kivuli cha Mwambusi kutoka vinywa vya mashabiki wa City.

Tukimpisha kocha huyo na sifa zake, kwenye sentesi nyingine Katibu Mkuu wa City Emmanuel Kimbe alisema ni kweli bechi la ufundi limeondokewa na mtu muhimu lakini suala la kutafuta mbadala linahitaji utulivu mkubwa ili kumpata mtu sahihi atakae kwenda sawa na utamaduni wa timu.

“Nakiri wazi kuwa aliyeondoka alikuwa mtu muhimu hasa ukizingatia alishiriki katika kuianzisha timu lakini kwenye soka ndivyo ilivyo, kitu muhimu kwetu kwa sasa ni utulivu huku tukisaka mtu sahihi atakayeweza kuendana na utamaduni wetu” alisema.

Ni utamaduni upi? Ni wazi City inahitaji kuendelea kuwa timu ya ushindani huku akisaka mafanikio zaidi kwenye soka la Tanzania kabla ya kugeukia kimataifa huku ikiwa na ‘lawi’ ya kuendelea kuwaibua na kuwatumia nyota wa kitanzania walio tele mitaani licha ya vipaji walivyojaliwa.

Kwa mashabiki wa City jambo zuri ni kuendelea kusubiri nini kitatokea kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa na maana kubwa alipoitengeneza kesho,huenda jina wanalolitaja litapita na kiu yao kuwa imekatika kama ambavyo ilikatika wakati wanasubiri timu yao kupanda daraja.

Lakini kwa sasa sentesi iliyopo kutoka uongozi wa City ni kuwa Kocha msaidizi Meja Mstaafu Abdul Mingange ataendelea kushika usukani wa kuongoza benchi la ufundi la timu ya kizazi kipya nyuma yake akiwa na Mohamed Kijuso na Rashird Kasiga.

“Kwa hiyo ni vyema tukaendelea kusubiri nini kitatokea, tunayo maombi mengi lakini kwa sasa hakuna kitakachobadirika kwa maana kuwa Kocha msaidizi Meja Mstaafu Abdul Mingange ataendelea na majukumu ya kuongoza timu sambamba na wasaidizi wake wengine Kijuso na Kasiga mpaka hapo itakapotolewa taarifa nyingine”
Hiyo ilikuwa ni kauli ya mwisho ya Katibu Mkuu Kimbe akipigilia msumari kuzima tetesi za kocha mpya wa City, licha ya kukiri kuwa tayari anazo kichwani taarifa za kupigiwa chapuo kwa kocha Phiri na mashabiki wa timu hii.

Ureno, Ujerumani, Ufaransa, Ghana, Ivory Coast, Malawi na Afrika Kusini ni baadhi ya nchi ambazo uongozi wa City tayari umepokea barua za maombi kutoka makocha kadhaa wanaomba nafasi ya kuliongoza bechi la ufundi la timu ya kizazi kipya.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe

Ngao ya Jamii sasa ni Simba na Yanga

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limebadilisha kanuni za mashindano za Ngao ya Jamii kutoka timu nne na sasa utaratibu utakuwa kama zamani. Bingwa wa Ligi Kuu bara atacheza na mshindi wa kombe la CRDB Cup "CRDB Federation Cup, na endapo kama bingwa wa ligi na CRDB atakuwa ni mmoja basi mshindi wa pili kwenye Ligi Kuu ya NBC atacheza mchezo wa ufunguzi wa ligi yaani Ngao ya Jamii.  Hivyo ni rasmi ufunguzi wa wa ligi kuu mchezo  wa "Ngao ya Jamii msimu huu 2025-2026 ni Yanga na Simba watakutana.

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

Na Prince Hoza AFISA Habari wa klabu ya Yanga SC Ally Shabani Kamwe alidiriki kuudanganya umma wa wapenzi wa soka hapa nchini kwamba hakuna timu yoyote hapa Tanzania kuwahi kuingia hatua ya nusu fainali ya vilabu Afrika. Kamwe alisema timu yake ya Yanga itakuwa timu ya kwanza nchini kuingia nusu fainali ya Afrika, Yanga ilikuwa inakaribia kabisa kutinga nusu fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika. Yanga ilianza vizuri ikiwa ugenini baada ya kuilaza mabao 2-0 timu ya Rivers United ya Nigeria, hivyo ilikuwa inasubiria mchezo wa marudiano uliofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kwa vyovyote Yanga walikuwa na uhakika wa kutinga nusu fainali kwani walihitaji sare yoyote ama ushindi wa aina yoyote. Hapo ndipo Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliamua kupiga vijembe kwa watani zake Simba SC na kuipotosha jamii kwa kudai kwamba Yanga itakuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia nusu fainali ya Afrika. Kamwe ameifuta hadi rekodi ya Simba kuwa timu ya kwanza Tan...